‎Mama lishe wapewa mbinu kujiendeleza kibiashara

MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi (VETA), imewataka mama na baba lishe kujiendeleza katika fani ya mapishi ili kuboresha biashara zao na kujitangaza.

‎‎Pia imewataka kutumia nishati safi ya kupikia wakati wa shughuli zao ili kuepuka magonjwa ya upumuaji yatokanayo na matumizi ya kuni na mkaa.

‎Hayo yamesemwa leo na mwalimu wa fani ya mapishi kutoka VETA Chang’ombe, Euphrasia Mushi  kwenye mashindano ya upishi wa chapati kwa mama lishe wa Wilaya ya Temeke, yaliyofanyika Viwanja vya Mbagala Zakiem, Dar es Salaam.

Advertisement

‎Mushi amesema kuwa katika mashindano hayo wamechagua kumdhamini mama lishe ambaye atashika nafasi ya tatu  kupata mafunzo ya miezi mitatu katika fani hiyo.

‎Amesema sababu za kuwataka kujiendeleza ni kupata vyeti ambavyo vitawasaidia kutambulika, kujitangaza na kupata fursa ambazo zitajitokeza nchini.

‎”Kujiendeleza kutamsaidia mama lishe kujua mapishi mbalimbali ambayo yatamsaidia katika kukuza kipato cha biashara zao. VETA kuna kozi za kupika  vitafunwa tupu na vyakula mchanganyiko,” ameeleza.

‎Pia amesema fani hiyo itamwezesha mama lishe kujua mbinu mbalimbali za upishi, umuhimu wa kuzingatia usafi wake na wa chakula kwa ajili ya kumlinda mlaji.

‎”Chapati zina upishi wa aina mbalimbali kuna za mbogamboga, hamira na zile za mafuta na chumvi na endapo utakosea katika vipimo na ukandaji,  utapata chapati ngumu zisizochambuka,” amesema.

‎Miongoni mwa washiriki katika mashindano hayo, Neema Mwang’onda amesema kuwa ameshiriki mapishi hayo kwa sababu anapenda kupika na kwamba ni fursa ya kujitangaza.

‎Mwang’onda amesema  mashindano hayo yana ushindani mkubwa kutokana na kuwepo kwa wanawake ambao wana ujuzi wa muda mrefu wa kupika chapati na kwamba anaamini atakuwa mshindi.

‎”Ninajiendeleza katika fani ya mapishi  VETA Chang’ombe lengo langu niweze kujiamini wakati wa kupika, kutengeneza vitu vizuri na kuwa bora zaidi kwa mapishi mbalimbali ambayo yatanisaidia katika kuimarisha biashara na kuongeza kipato,” amesema Mwang’onda.

‎Naye, Stahimil Kasola  amesema baada ya kumaliza Kidato cha nne, aliamua kusomea fani ya uokaji na sasa anajifunza mapishi mchanganyiko kwa lengo la kufungua mgahawa wake.

‎Amesema kuwa ameshiriki kwenye mashindano hayo kwa sababu anaamini anaweza.