Mama wa kijana aliyeuawa aiomba serikali kusimamia kesi

MAMA mzazi wa marehemu Enock Mhangwa, Kulwa Baseke ameomba serikali imsaidie kuhakikisha inasimamia kesi ya kifo cha mtoto wake ili haki ipatikane.

Kulwa alieleza hayo juzi nyumbani kwake Uyovu mkoani Geita wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya mazishi ya mtoto wake.

Akisimulia tukio hilo alisema Juni 23, mwaka huu majira ya saa saba mchana alipigiwa simu na Mtendaji wa Kijiji cha Iyovu na kumuuliza kama anamfahamu Enock alimjibu ndiyo ni mtoto wake na kumtaka afike ofisi za kata ambapo mtoto anashitakiwa kwa wizi wa kompyuta.

“Niliwauliza Enock mpo naye, alinijibu ndiyo kwa sababu nilikuwa hospitali na mtoto wangu mwingine ambaye alikuwa mgonjwa nikawaambia hapa nipo nachukua huduma ya mtoto nikimalizia nakuja. Tulipofika nyumbani nikamwambia mtoto atenge chakula tule ili niende ofisini kabla sijaanza kula mtendaji alinipigia na kuniambia njoo umuage mwanao,’’ alisema Kulwa.

Alisema nilifikiria kuwa mtendaji amemuita aende ofisini lakini mbona anampigia simu akamchukue mtoto wake ndipo alimuuliza mtendaji kuwa wapo wapi alimjibu wapo pori la sekondari karibu na Roma.

Alieleza kuwa wakati anajiandaa kwenda ghafla watendaji wawili, mgambo wawili na watu wengine ambao hawafahamu walifika nyumbani hapo wakiwa na kijana wake akiwa amepigwa sana.

“Nilitetemeka moyo ulikuwa unaogopa, Enock alikuwa ameanguka mlangoni wakamvuta hadi ndani huku wakimlazimisha aongee, nilimuuliza Enock kwa sababu nyie ni vijana labda utakuwa ulichukua vitu sema vilipo, Enock alinijibu mama sijaiba chochote nimewaleta hapa ili unisaidie mama wamenipiga sana,’’ alisema.

Kulwa alisema watendaji hao walimtaka alipe Sh 200, 000 nikawaambia sina hiyo fedha na siwezi kuwalipa kwa sababu wameshampiga mwanangu na hali aliyonayo ni mbaya; alikuwa hawezi kukaa, alikuwa amelala tu huku akiomba maji.

“Waliniambia nisimpe maji wameshampiga mno anaweza kukata moto hapa pia wakasema tumeshajua kumbe huyu alituambia tumlete nyumbani kwao ili apate msaada wakamwambia nyanyuka twende akawa hawezi wakampiga tena akanyanyuka wakaondoka naye. Nikaenda kituo cha polisi wakadai kuwa Enock aliletwa pale walimkataa kwa sababu ya hali aliyokuwa nayo,’’ alisema.

Mama huyo alieleza kuwa aliamua kwenda kumtafuta hospitali alikuta Enock ameshafariki na mwanae kabla ya kufariki alimwambia waliokuwa wakimpiga ni watendaji wa kata na mgambo.

Aidha, alisema hakuwahi mapema ofisini kwa mtendaji licha ya kuwa hospitali kwa sababu alikuwa akijua mtoto wake yupo sehemu salama.

Imeandikwa na Yohana Shida (Geita) na Rehema Lugono (Dar).

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button