Mama wa watoto 4 waliovunjika miguu ajalini asimulia

MKAZI wa Dodoma, Salama Omary ni miongoni mwa abiria waliokuwa katika ajali ya basi Super Najimunisa na kusababisha watoto wake wanne kuvunjika miguu.

Basi hilo lenye namba za usajili T 413 DAY likitokea Dar es Salaam kwenda jijini Mwanza pia limesababisha vifo vya watu watano na wengine 56 kujeruhiwa baada ya kugongana uso kwa uso na Fuso eneo la Ibadakuli, Manispaa ya  Shinyanga.

Salama akiwa ni miongoni mwa abiria waliokuwa kwenye basi hilo, alieleza kuwa alikuwa akisafiri na watoto watano lakini baada ya ajali hiyo watoto wake wanne wamevunjika miguu na mmoja ndiyo mzima.

Advertisement

Alidai kuwa alikuwa akimfuata mumewe aliyehamishiwa kikazi Serengeti mkoani Mara.

“Nilikuwa nimelala nikashtukia gari limesimama nimebanwa, watoto siko nao kwenye siti huku wakilia na kuniita nikaamka na kuanza kuwavuta kumbe wamevunjika miguu watoto wote wanne na mmoja mzima na mimi nimepata majeraha kidogo,” alisema Salama.

Shuhuda, Fred Mahina alisema kuwa dereva alikuwa mwendo kasi walipofika Morogoro alitozwa faini lakini aliendelea hivyo na njiani alisimamishwa mara nyingi na askari wa usalama barabarani kabla ya kupata ajali mkoani Shinyanga.

“Tulipofika Morogoro dereva akiwa mwendokasi, alikwaruza lori tukapona kuanguka, lakini akazidi kuendesha mwendokasi, abiria tulipokuwa tukipiga kelele apunguze mwendo, aligoma na kutuambia tusali na kama tungetaka usafiri wa raha tungepanda ndege,” alisema Mahina.

Kaimu Kamanda wa Polisi, Leonard Nyandahu aliyekuwa katika eneo la ajali alisema kuwa ajali hiyo imetokea jana usiku na kuwa watu watano wamekufa  na 56 wamejeruhiwa.

“Kwa taarifa iliyopo ni basi la Super Najimunisa lenye namba za usajili T413 DAY likitokea Dar es Salaam kuelekea jijini Mwanza, liligongana na gari aina ya  Fuso yenye namba za usajili T123 DJH likitokea Mwanza kwenda Dar es Salaam likiwa na mzigo wa dagaa,” alisema.

Kamanda Nyandahu alisema kuwa ajali hiyo imetokea kwa sababu ya uzembe wa dereva wa kutozingatia sheria za usalama barabarani kwa kuendesha mwendokasi.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jansita Mboneko alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi na usiku taa zinakuwa na mwanga mkali. Aliwasihi madereva kuwa makini barabarani.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Dk John Luzila alithibitisha vifo vya watu watano akiwemo mtoto wa miaka sita.

“Mpaka sasa majina ya marehemu hayajafahamika, miili imehifadhiwa  katika chumba cha kuhifadhia maiti na majeruhi wanaendelea kupata matibabu,” alisema Dk Luzila.