Mamba aua mwanafunzi akivua samaki

MWANAFUNZI wa darasa la sita, Shule ya Msingi Ugala iliyopo Halmashauri ya Nsimbo mkoani Katavi, Msopola Issa (14) amefariki baada ya kushambuliwa na mamba wakati akivua samaki kwa kutumia ndoano Mto Ugala.

Akithibitisha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Ali Makame alisema mkasa huo ulitokea Machi 19, 2023 majira ya saa nane mchana wakati mtoto huyo akivua samaki katika mto huo.

Akisimulia kisa hicho, Mwenyekiti wa Kijiji cha Ugala, Shaban Juma alisema mchana huo wa tukio mwanafunzi huyo wakati akivua samaki mtoni ghafla alishambuliwa na mamba hadi kumsababishia umauti.

“Mamba huyo aling’ata mguu wa mtoto huyo ambaye alikuwa akilia akiomba msaada, wakiwa na silaha mbalimbali za jadi baadhi ya wanaume waliosikia mtoto huyo akipiga yowe walikimbilia eneo la tukio, lakini walikuwa wamechelewa kwani mnyama huyo alikuwa tayari amemvuta mtoto huyo kwenye kina kirefu cha maji,” alisema.

Alisema muda huo baadhi ya wanaume kwa ujasiri walipiga mbizi mtoni kitendo kilichomwogofya mnyama huyo ambaye alikimbia na kuuacha mwili wa Msopola ukielea majini.

Aliwataka wananchi wanaoishi katika vijiji vilivyo jirani na mto huo kuchukua tahadhari mbalimbali, ikiwemo kuoga nyumbani badala ya kuogelea kwenye mto huo ambao una idadi kubwa ya mamba.

Habari Zifananazo

Back to top button