Mambo mazuri ukarabati Chuo Kikuu Butiama

UKARABATI wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius  Kambarage Nyerere Cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT) Kampasi ya Oswald Mang’ombe,  wilayani Butiama, Mkoa wa Mara umeanza kwa ajili ya kuanza kupokea wanafunzi awamu ya kwanza, mwaka huu wa masomo 2023/24.

Ukarabati huo unaohusisha madarasa nane,  maabara mbili, bwalo la chakula, kubadili jengo la mkutano kuwa maktaba na kubadili nyumba moja kuwa zahanati utakamilika ndani ya wiki mbili zijazo.

Mradi huo unaenda sambamba na ujenzi wa miundombinu mipya ya madarasa 60 na bweni lenye uwezo wa kubeba wanafunzi 112, amesema Makamu Mkuu wa chuo, Prof Benard Melau, wakati wa ziara ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Adolf Mkenda.

Advertisement

“Tunaishukuru serikali kutenga zaidi ya Shilingi billioni 2.6 kwa ajili ya mradi huu. Tayari tumepokea Shilingi billioni moja. Zaidi ya Shilingi millioni 580 zimeshatumika kununua vifaa vya ukarabati na kwa ajili ya kulipa mafundi.

“Tunasubiri kupokea kiasi kilichobaki tuanze ujenzi wa majengo mapya. Miundombinu yote itakua tayari kabla ya udahili na kwa kuanzia tutakua na wanafunzi takribani 300,” amesema.

Amesema kwa kuanzia Kampasi itatoa kozi tatu kwa ngazi ya Shahada, ambazo ni Uchumi na Biashara ya kilimo, Kilimo cha samaki pamoja na Sayansi ya Kompyuta.

Waziri Mkenda amepongeza jitihada za ukarabati na mpango wa kuanza na kozi chache,  akakitaka chuo kutojirundikia mambo mengi kwa wakati mmoja, ambayo yanaweza kuathiri ubora wa mazao yake.

 

2 comments

Comments are closed.

/* */