RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema uadilifu na weledi kazini ndio utaleta maisha bora kwa wafanyakazi na kusema kuwa hatatangaza hadharani suala la kupandisha mshahara, lakini amewaeleza wafanyakazi kuwa mambo mazuri yapo na kwamba mambo ni moto.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani mwaka 2023, yaliyofanyika kitaifa mjini Morogoro , 2023, Rais Samia amesema kujitoa kwa wafanyakazi kwa bidii kutasaidia kulijenga Taifa.
“Kauli mbiu ya mwaka huu Mishahara Bora na Ajira za Staha ni Nguzo kwa Maendeleo ya Wafanyakazi. Wakati ni Sasa…. “
“Kauli mbiu hii inalenga kuimarisha na kuboresha maslahi ya wafanyakazi. Nami naongeza kauli mbiu inavyosema, uadilifu na weledi kazini ndio utaleta maisha bora kwa wafanyakazi.
“Kujitoa kwetu (wafanyakazi) kwa bidii kunasaidia kujenga Taifa, kuna kazi kubwa ya wafanyakazi. Sisi wafanyakazi tuna mchango mkubwa katika Taifa hili,”amesema.
Akizungumzia nyongeza ya mishahara na posho, Rais Samia amesema zipo taasisi ambazo zilishindwa kutekeleza agizo la kutoa nyongeza za psoho kwa kuwa wakati anatoa agizo hilo bajeti ilikuwa imeshapita, kwa maana hiyo mavuno ya posho hizo yatakuwa kwenye bajeti ya mwaka huu, 2023/2024.
Amesema, mbali na upandishaji wa posho, mwaka huu pia ataendelea kupandisha madaraja, vyeo na madaraja mserereko upo mwaka huu.
“Lakini niseme pia kuna nyongeza za mishahara ambazo muda mrefu zilisitishwa, nimeona mwaka huu tuzirudishe. Kwa hiyo wafanyakazi wote mwaka huu nyongeza za kila mwaka zitakuwepo na itakuwa hivyo kila mwaka.
“Nashukuru Tucta mwaka huu wamenielewa hawakuja na mdomo mkali wa moto mara hii wamekuwa wapole, kwa hiyo waliyozoea nitangaze hapa ili wajue kiasi gani, ili wapandishe bei madukani sitatangaza, ili mwenendo wa bei uwe salama, tutapandisha pole pole mambo mazuri yapo ila hatutayatangaza hapa, mambo ni moto, mambo ni fire,”amesisitiza.
Aidha, kuhusu kilio cha kodi na marupurupu ya makato kwa wakati pamoja hadi zawadi zinakatwa kodi, ameelekeza Waziri wa Utumishi na Waziri wa Fedha kukaa kuangalia yale yanayopaswa kukatwa kodi yakatwe na yasiyofaa yaondolewe.
“Leo nimeshuhudia mtu anatoka na milioni 12 hapa kwa nini asikatwe kodi, hiyo kodi itarudi kwenye kufanya shughuli nyingine, hivyo naliacha kwa Waziri wa fedha na Waziri wa Utumishi yanayopaswa kulipa kodi yalipwe yanayofaa kuondolewa yaondolewe,”amesisitiza Rais Samia.
Kuhusu waajiri wa kutopeleka michango katika mifuko ya jamii na michango ya bima za afya, Rais Samia amemuagiza Waziri Mkuu kushughulikia suala hilo na kuhakikisha waajiri wote wanawasilisha michango ya wafanyakazi wao.
Pia ametoa siku 60 kwa waajiri kulipa malimbikizo ya bima za afya, ili wafanyakazi wao waweze kupata stahiki zao za matibabu.
“Malimbikizo yote ya bima ya afya yalipwe ndani ya siku 60 kama kuna mtu analimbikiza atajua mwenyewe ndani ya siku 60 ziwe zimelipwa waajiriwa waweze kupata haki zao,”amesisitiza Rais Samia.