Mambo yaiva mradi wa gesi asilia

WIZARA ya Nishati imebainisha kwamba mwezi ujao serikali inatarajia kusaini mkataba wa kuanza Mradi wa Kuchimba Gesi Asilia (LNG) katika eneo la Bahari Kuu Kusini mwa Tanzania.

Imesema mradi huo ni habari njema kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zitakapokutana katika Kongamano la Mafuta na Gesi la Afrika Mashariki litakalofanyika Mei 9 hadi 11, mwaka huu nchini Uganda.

Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato alisema hayo Dar es Salaam jana katika kikao na wadau mbalimbali wa sekta ya mafuta na gesi kilichojadili namna Tanzania itakavyoshiriki na kunufaika katika kongamano hilo.

Byabato alisema mpaka sasa Tanzania imefanya vizuri katika sekta ya gesi kwani asilimia 60 hadi 70 ya umeme unaozalishwa Tanzania ambao ni megawati 1,900 unatokana na gesi hali inayoifanya nchi kuwa mfano wa kuigwa Afrika Mashariki na Kati.

“Jambo kubwa tunaloenda nalo katika mkutano huo ni kuwapa taarifa njema za maendeleo ya mradi wetu wa LNG tunaoufanya katika eneo la Bahari Kuu, ambapo tukiivuna ile gesi tutaileta katika eneo linaitwa Likong’o pale Lindi kwa ajili ya kuichakata,” alieleza Byabato.

“Tunaamini mwezi unaokuja Mwenyezi Mungu akijalia tutasaini mkataba kati yetu na wabia ambao tulikubaliana nao kutekeleza mradi huu na tutakamilisha jambo hili la majadiliano na kuingia ‘site’ na kuanza kuchimba gesi hiyo,” aliongeza Byabato.

Alisema Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na wadau wengine kama Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Mamlaka ya Udhibiti na Utafutaji wa Mafuta na Gesiasilia Zanzibar (ZPRA) watakuwa na jukumu la kutangaza fursa zitokanazo na mradi huo mkubwa wenye thamani ya Sh trilioni 70 kwa wawekezaji na wafanyabiashara kutoka katika mataifa mbalimbali barani Afrika.

Alisema mbali na mradi huo mkubwa, Tanzania itaendelea kuwavutia nchi wanachama wa EAC kwenye sekta ya gesi na kuongeza kuwa taifa limejipanga kupeleka gesi kwa nchi zilizoonesha kuvutiwa na gesi hiyo kama Kenya, Rwanda, Zambia na Uganda.

Alisema Tanzania ni nchi ya amani hivyo uchimbaji na usafirishaji wa nishati hiyo ni salama kiasi mataifa yote hayatakiwi kujiuliza mara mbili kuhitaji nishati hiyo.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Joyce Kisama alisema mbali na kongamano la Uganda, Tanzania ina nafasi nyingine nzuri ya kunadi miradi mbalimbali ya gesi katika kongamano litakalofuata mwakani ambalo litafanyika Tanzania.

Mdau na msafirishaji wa mafuta ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya MOIL, Altaf Manson aliwataka wafanyabiashara na wawekezaji wa Tanzania kuchangamkia fursa zinazotokana na kongamano hilo.

Alisema kwa Watanzania ambao wataona uwezo wao ni mdogo ni bora waungane ili wapate nguvu ya kushiriki. Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa ZPRA, Abdulkadir Mahmoud Juma alisema wamejipanga kushiriki kikamilifu kongamano hilo kwa kuwa wana malengo ya kuifungua Zanzibar katika sekta ya mafuta na gesi.

Alisema yapo maeneo ya Bahari Kuu yanatakiwa kufunguliwa kwa kutangazwa kuwavutia wawekezaji na wafanyabiashara kuja kuwekeza katika visiwa hivyo.

Habari Zifananazo

Back to top button