Mambo yaiva ujenzi SGR Tanzania, Burundi

MCHAKATO wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Tanzania hadi Burundi umeanza kufuatia kutangazwa kwa zabuni ya ujenzi wa reli hiyo yenye urefu wa kilometa 282.

Tangazo la zabuni hiyo limetolewa na Tanzania na Burundi kwa ajili ya usanifu na ujenzi wa reli ya kisasa ya umeme chini ya Mradi wa Kimataifa wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa wa Tanzania –DRC, awamu ya kwanza.

Mradi huo unatekelezwa kutoka Uvinza mkoani Kigoma hadi Kindu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kupitia Gitega nchini Burundi.

Tanzania na Burundi ziliingia makubaliano ya ujenzi huo na kuteua Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuwa wakala wa utekelezaji wa mradi huu wa kimataifa.

Katika tangazo la zabuni lililotolewa na kuthibitishwa na TRC, imeeleza kuwa zabuni hiyo ni usanifu na ujenzi wa takribani kilometa 282 za reli hiyo ya kisasa ya umeme kutoka Uvinza Tanzania (kwenye makutano ya reli ya kisasa ya Tabora hadi Kigoma) kupitia katika mpaka wa kimataifa katika Mto Malagarasi mpaka Musongati na Gitega nchini Burundi.

Kwa mujibu wa tangazo hilo, zaburi hiyo inatakiwa kuwasilishwa kabla ya Mei 15, mwaka huu saa 4:30 asubuhi katika makao makuu ya TRC.

Inaelezwa kuwa ujenzi wa reli hiyo umepangwa katika maeneo mawili, kwanza kilometa 156 katika upande wa Tanzania na kutekelezwa mara moja.

Eneo la pili kwa mujibu wa taarifa, ni kilometa 126 eneo la Burundi na utatekelezwa mara mbili.

Kwa upande wa Burundi, taarifa zinasema, itakuwa na ujenzi wa Malagarasi mpaka Musongati kilometa 80 na Musongati mpaka Gitega kilometa 46.

TRC kwa kushirikiana na ARTF ambalo ni shirika la Burundi linalosimamia masuala ya reli, watajenga takribani kilometa 282 za reli kati ya Uvinza na Gitega kupitia Musongati Burundi na njia nyingine za reli ya kisasa chini ya viwango vya kimataifa.

Mradi huo utatekelezwa kwa muda usiopungua miaka mitano katika usanifu kwa Dola za Marekani milioni 20 huku ujenzi ukiwa kwa muda wa wastani wa miaka mitano kwa Dola za Marekani bilioni moja.

Novemba mwaka jana, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango alisema kutekelezwa kwa mradi huo kutoka Uvinza mkoani Kigoma hadi Kindu, DRC kupitia Gitega nchini Burundi kutaongeza ufanisi katika matumizi ya Ukanda Huru wa Biashara barani Afrika kwa kuimarisha usafirishaji wa watu na bidhaa.

Dk Mpango alisema hayo wakati akiongoza majadiliano na wawekezaji kuhusu mradi wa reli hiyo ya kisasa yaliyofanyika katika Jukwaa la Uwekezaji barani Afrika jijini Abidjan, Ivory Coast.

Alisema serikali zote tatu zimeweka nia ya dhati ya kutekeleza mradi huo ambapo kwa upande wa Tanzania tayari imekwisha tekeleza miradi unganishi ya reli ya kisasa inayochagiza uwepo wa mradi huo muhimu.

Aidha, Makamu wa Rais alisema asilimia 50 ya mizigo inayotoka katika bandari za Tanzania hupelekwa nchi za Burundi na Congo hivyo uhitaji wa reli hiyo ya kisasa ni muhimu kwa sasa.

Kwa upande wake, Waziri wa Miundombinu wa Burundi, Dukundane Dieudonnee, alisema taifa hilo limekuwa likipoteza zaidi ya Dola za Marekani milioni 17 kwa mwaka katika usafirishaji wa mizigo hivyo mradi huo utasaidia katika kukabiliana na hali hiyo.

Mei mwaka jana nchi za Tanzania, Burundi na DRC, ziliwasilisha maombi ya kupatiwa mkopo wenye masharti nafuu kwenye Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa ajili ya SGR kutoka Uvinza-Msongati- Gitega, yenye urefu wa kilometa 939, uliokisiwa kugharimu Dola za Marekani milioni 900.

Habari Zifananazo

Back to top button