MKOA wa Manyara umetangaza kuanza kliniki maalum ya kwanza ya madaktari bingwa wa ndani ya mkoa huo kutoa huduma bobezi za kitabibu za magonjwa mbalimbali ya wanawake na watoto.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amesema hayo leo November 18 ambapo mkoa umebuni mkakati huo maalum kutokana na mahitaji makubwa ya kimatibabu kwa wananchi.
“Tunakwenda kuongeza uchunguzi wa mapema wa magonjwa mbali mbali kabla hayajakuwa sugu ili wananchi waweze kuondokana na kadhia kubwa ya magonjwa kuwa sugu kwasababu ya kutokupatiwa tiba ama kuonwa na madaktari bingwa haraka Katika hatua za magonjwa ya awali lakini kingine tunakwenda kuwajengea uwezo watumishi wa afya katika hospitali zetu zote za wilaya kwakutumia madaktari bingwa,” amesema RC Queen Sendiga.
Amesema timu ya madaktari itaweka kambi sehemu moja: “Tunaweka kambi siku kadhaa sehemu hiyo ambayo tunahakikisha kwamba wagonjwa hao wote wa kwenye maeneo hayo na maeneo jirani watapata tiba.”
Wakati mpango huo ukianza kutekelezwa serikali inawasisitiza wanawake kuhudhuria kliniki kulingana na ushauri wa madktari ili kujiepusha na hatari ya kupatwa na magonjwa yanayopelekea vifo vya wajawazito ikiwemo kifafa cha Mimba.
“Lakini utaona katika madaktari ambao tunawataja wapo wataalamu bingwa wa usingizi kutoa dawa za ganzi sasa wale wataenda kuwajengea uwezo pia wale wataalamu wetu wa ngazi ya halmashauri ili waweze kutoa dawa zile hata kwa kesi ambazo mwanzoni walikuwa hawawezi kutoa kwasababu mashine zimepelekwa ambazo zinaweza kufanya hivyo sasa wakifanya namna hiyo utaona kuna wagonjwa ambao baadaye wangekuja kupata rufaa kuja hospitali ya mkoa,” ameongeza.
RC Sendiga amesema kuwa: “Kama unajua mfano Simanjiro kilometers takribani hata 200 sasa hao hawatapewa tena rufaa kwa sababu watatibiwa kule na hawa madaktari wataalamu wa usingizi watakaojengewa uwezo pale maana yake wataweza kupata ujuzi wa matumizi sahihi ya dawa za usingizi na ganzi na badala yake tutapunguza idadi ya rufaa ambazo zinaletwa katika hospitali yetu ya mkoa.”