Maofisa afya watakiwa kusimamia usafi wa mazingira

KAIMU Mkurugenzi Idara ya Kinga katika Wizara ya Afya, Dk Beatrice Mtayoba amewataka maofisa afya wote jijini Dodoma kusimamia usafi wa mazingira ili kupunguza maambukizi ya magonjwa ya mlipuko kwa asilimia 70.

Dk Mtayoba alisema hayo jijini hapa wakati alipotembelea Soko la Bonanza lililopo katika Kata ya Chamwino akiongozana na Meya wa Jiji la Dodoma, Profesa Davis Mwamfupe, Diwani wa Kata ya Chamwino, Jumanne Ngede, maofisa afya na kufanya usafi katika eneo hilo la soko.

Mtayoba alifanya usafi pamoja na wafanyabiashara na wananchi wa maeneo hayo ikiwa ni kuadhimisha wiki ya usafi wa mazingira kitaifa ambayo imeanza Novemba 15 na kilele chake kitakuwa kesho.

Advertisement

Alitaka maofisa hao kusimamia usafi kwa kuhakikisha kuna miundombinu ya usafi kwenye maeneo yote ya masoko kwenye taasisi, kaya na miundombinu ya vyoo bora na watu wavitumie pamoja na kuweka miundombinu ya kunawia mikono kwa maji tiririka na sabuni.

Aidha, alisisitiza maofisa hao kusimamia usafi pembeni ya kaya 500, kwenye mitaro, taasisi kwenye shule na kuhakikisha kila mtu angalau meta tano inayozunguka eneo lake linakua safi pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kutumia vyombo vya habari.

“Siku tulizotenga za Jumamosi kufanya usafi, tuna mabwana afya, tuna watendaji wa kata lakini kila eneo la Jiji lina mwenyewe.

“Kila eneo tunalopita, kuna mwenye nalo. Mfano hapa mbele ya duka hili, kuna mtaro ambao mwenye duka sasa ausimamie.

“Tukisimamia vizuri, tutajikuta hata kazi zile za Jumamosi ya kila mwisho wa mwezi, zinakua sio nzito,” alisema.

Alisema usafi wa mazingira ndiyo kila kitu kwani hata ugonjwa wa kipindupindu mara zote unasababishwa na kutokuwa na mazingira safi.

Kwa upande wake, Meya wa Jiji la Dodoma, Profesa Davis Mwamfupe alitaka wafanyabiashara wote wa soko hilo ambao maduka yao mbele kuna mtaro na wameweka makalavati kuyatoa, badala yake waweke madaraja ya chuma kwani makalavati yanafanya taka kujificha chini na kushindwa kufanya usafi.

“Watu wote walioweka makalavati humo kwenye mitaro myavunje, viongozi mlioko hapa mhakikishe kufikia Jumamosi tutakapopita tena, yawe yamevunjwa badala yake muweke vile vidaraja vya chuma ili tuweze kupitisha takataka chini,” alisema.

Pamoja na hayo, Profesa Mwamfupe alisema Halmashauri ya Jiji la Dodoma limeingia mkataba na kampuni kutoka Zimbabwe ambayo lengo lake litakuwa ni kuchakata taka na kupata gesi na mbolea.

Naye Diwani wa kata hiyo, Jumanne Ngede alisema usafi ni jukumu la kila mwananchi na kuahidi kuendelea kufanya usafi kama ambavyo wamefanya jana.