Maofisa TRA mbaroni leseni feki za udereva

Maofisa TRA mbaroni leseni feki za udereva

JESHI la Polisi Mkoa wa Iringa linawashikilia wafanyakazi wawili wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Iringa, Upendo Msigwa (32) mkazi wa Mawelewele na Chali Chaliga (28) mkazi wa Donbosco mjini Iringa kwa tuhuma za kushirikiana na watuhumiwa wengine watatu kutoa leseni za udereva kinyume na sheria na taratibu za nchi.

Watuhumiwa hao watatu ambao ni wafanyabiashara wanaoishi katika maeneo tofauti mjini Iringa ni pamoja na Omary kibao (38) mkazi wa Kitwiru, Johnson Kihongosi (31) mkazi wa Zizi la Ng’ombe na Dikson Nelson (32) mkazi wa Feelimo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Iringa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa ACP Allan Bukumbi, alisema watuhumiwa hao walikamatwa baada ya jeshi la Polisi kupokea taarifa za uhalifu huo kutoka kwa wasamaria wema.

Advertisement

“Tarehe 16 mwezi huu wa pili majira ya saa 3.00 asubuhi tulipokea taarifa kwamba katika mtaa wa Mahiwa mkabala na ofisi ya TRA Mkoa kuna wafanyabiashara wa duka la vifaa vya maofisini wanashirikiana na maafisa wa TRA kutoa leseni za udereva kinyume cha sheria,” alisema.

Baada ya kupokea taarifa hiyo alisema waliunda timu ya upelelezi na kufanikiwa kumnasa Kihongosi, Kibao na Nelson ambao baada ya kufanyiwa upekuzi walikutwa na leseni za udereva 31, vitambulisho vya Nida na mpiga kura vinne, nakala za kadi za magari ya watu mbalimbali na Police loss reports.

Aidha Kamanda Bukumbi alisema  watuhumiwa hao walikuwatwa pia na namba za magari na Pikipiki 431,TIN namba nane, printer tano, laptop moja, kompyuta ya mezani moja, nakala za vyeti vya mafunzo ya udereva viwili, scanner moja na  lamination mashine moja.

Alisema baada ya watuhumiwa hao kuhojiwa na kukiri kufanya uhalifu huo waliwataja maafisa hao wawili wa TRA kwamba ndio wamekuwa wakishirikiana nao kujipatia fedha kinyume cha sheria na kuipotezea serikali mapato yake halali.

Wakati wakiendelea na uchunguzi wa tukio hilo, wakati wakijipanga kuwafikisha watuhumiwa hao mahakamani alisema, watawatafuta watu wote ambao waliomba leseni hizo kinyume na mifumo halali ya nchi pamoja na wamiliki wa magari ambayo namba zake zilikutwa kwa watuhumiwa hao.

“Tutawatafuta watu hao ili watusaidie kujua utaratibu walioutumia kujipatia leseni na namba hizo za magari kupitia kwa watuhumiwa hao badala ya mamlaka rasmi zinazotambulika na serikali,” alisema.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *