Maofisa ugani wapewa pikipiki kuimarisha uzalishaji pamba

MWANZA; MAOFISA ugani 12 kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza, wamekabidhiwa pikipiki 12 kwa ajili ya kusimamia zao la pamba katika wilaya hiyo, ikiwa ni sehemu ya kuboresha huduma za ugani na kuongeza uzalishaji wa zao hilo.

Akikabidhi pikipiki hizo,  Katibu Tawala wa Wilaya ya Kwimba, Mohamed Ngasinda, amewataka maofisa ugani kuzitumia kwa umakini  na uadilifu,  ili kuimarisha usimamizi wa zao la pamba.

Ngasinda amesema kuwa serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha zao hilo linafufuliwa ili kuongeza tija.

“Juhudi zilizopo ni kurudisha uhai wa zao la pamba kwa kuliboresha kupitia mbegu bora, mbolea na uwepo wa wataalamu wa kusimamia maendeleo yake,” alisema Ngasinda.

Amewataka maofisa ugani hao kufanya kazi kwa bidii na kuonesha weledi, ili kuongeza uzalishaji na kufikia malengo ya serikali ya kulihuisha zao hilo.

“Msibadili matumizi ya pikipiki hizi kwa shughuli nyingine. Pikipiki hizi zinapaswa kutumika kusimamia maendeleo ya zao la pamba. Tunataka muwe kiungo muhimu cha kufanikisha malengo ya kuongeza uzalishaji,” alisisitiza.

Amewataka maofisa ugani kwenda kuhamasisha wananchi kulima zao la pamba. Amesema Serikali inaendelea kutoa mbegu na mbolea kwa bei ya ruzuku ili kuongeza ushiriki wa wakulima katika kilimo cha pamba.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button