ZAIDI ya wachimbaji wadogo 2,000 wameanza maonesho ya bidhaa zao yatakayodumu kwa wiki moja jijini hapa, huku wakielezea maendeleo yanayofanyika katika sekta kuongeza uzalishaji.
Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo nchini (FEMATA), John Bina, amesema jitihada za kuondokana na teknolojia za zamani, ikiwemo matumizi ya zebaki, ni sehemu ya maendeleo hayo, kwani mbali na athari zingine, (zebaki) inazorotesha uzalishaji kwa kukosa uwezo wa kumaliza dhahabu katika udongo, wakati wa uchenjuaji.
“Hivyo tunaongeza bidii jitihada kuhamia teknolojia za kisasa, ikiwemo ‘CIL’ na ‘CIP’, zenye uwezo wa kuondoa madini yote katika udongo.
“Tumealika wachimbaji kutoka nchi mbalimbali za Afrika tubadilishane uzoefu. Tunaamini matumizi ya zebaki yataisha kabisa ifikapo mwaka 2030, kama ilivyo azma ya serikali,” amesema.
Mkurugenzi Kampuni ya uhandisi TIES, Mhandisi Josia Komogo, anasema tayari kampuni hiyo imeanzisha teknolojia ya CIL, ili kuwaepusha wachimbaji wadogo na athari za zebaki.
Amepongeza serikali kuendelea kukuza viwanda vya ndani, ambavyo vinazalisha malighafi za CIL nchini, hatua inayoiwezesha TIES kufunga mitambo ya kuchenjulia dhahabu kwa bei nafuu.
Alisema CIL si tu inaongeza uzalishaji kwa kuondoa dhahabu yote katika udongo, bali pia inafupisha muda wa uzalishaji, kutoka zaidi ya wiki mbili kwa matumizi ya teknolojia za zamani, hasa zebaki na ‘vat-leaching’, hadi saa takribani 30 tu.