SHILINGI bil 1.2 za mapato ya ndani Manispaa ya Morogoro zimetumika kujenga kituo cha afya Kata ya Tungi. Kituo hicho kitakachokuwa na zana za kisasa za huduma za matibabu kitahudumia watu takribani 16,793 wanaoishi katika kata hiyo na jirani.
Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Ally Machela alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea kujionea shughuli za ujenzi wa kituo hicho. Machela alisema kituo hicho kinajengwa kwa kufuata maelekezo ya Wizara ya Afya na kina majengo 10 ya kutolea huduma mbalimbali na katika hatua ya kwanza ujenzi wake umetumia Sh milioni 350.
“Kwa sasa tupo katika hatua ya upauaji na tayari tumelipa fedha Sh milioni 83 za ununuaji wa bati na bati hizo wametuahidi wiki ijayo kiwanda kitaleta hizo bati,” alisema Machela. Alisema mradi huo wa ujenzi katika Kata ya Tungi umekuwa ni ukombozi mkubwa kwa wananchi wake na wengine wa kata za jirani kupata huduma za afya eneo la karibu.
“Malengo ya Manispaa yalikuwa ni kujenga kituo cha afya ambacho kimetimia na kwa ujumla tumekidhi vigezo vyote vya majengo yote yanayotakiwa kwa ajili ya mradi wa afya,” alisema Machela. Alisema majengo hayo yatawekewa njia maalumu za kupita wagonjwa na watoaji wa huduma katika kituo hicho.
Pia alisema Manispaa hiyo inajenga kituo cha afya kingine kinachotokana na fedha za tozo katika Kata ya Lukobe na kitakapokamilika kitatoa huduma kwa asilimia 100 na sasa kipo katika umaliziaji.
Naye Mganga Mkuu wa Manispaa hiyo, Charles Mkombachepa alisema kituo hicho cha afya cha kisasa kina majengo hayo 10 ya kutolea huduma ambayo ni jengo la wagonjwa wa nje (OPD), jengo la akina mama wajawazito, jengo la maabara, jengo la upasuaji akina mama wajawazito, jengo la akina mama wajawazito wanaojifungua na wenye shida mbalimbali za uzazi.
Mganga mkuu wa Manispaa hiyo pia alisema kituo hicho cha afya kina nyumba moja ya mtumishi, jengo la kufulia nguo pamoja na jengo la kuhifadhia maiti