Marais saba kuja mkutano wa kahawa Afrika kesho

MARAIS saba wamethibitisha kushiriki mkutano wa nchi 25 zinazolima kahawa Afrika (G-25) unaotarajiwa kufanyika kesho na keshokutwa kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Nyerere (JICC) Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania, Primus Kimaro alisema Dar es Salaam kuwa mkutano huo utaanza kwa kukutanisha mawaziri wa nchi hizo kesho kabla ya marais kukutana keshokutwa.

“Mpaka sasa wakuu wa nchi saba wamethibitisha kushiriki, nchi nyingine zitakuwa na wawakilishi tu na maandalizi ya kuwapokea na mkutano huo kwa ujumla yanaendelea vizuri,” alisema Kimaro.

Advertisement

Alisema lengo la mkutano huo ni kukuza thamani ya kahawa na kujadili changamoto zinazokabili zao hilo lakini pia, kutumia fursa za kupata ajira hasa kwa vijana.

“Tunatarajia changamoto za sekta ya kahawa Afrika zitatatuliwa hasa kwa kuangalia ajira kwa vijana kupitia uboreshaji wa sekta ya kahawa na ni matumaini yetu kahawa ya Afrika itaboreshwa, itaongezwa thamani na itatumika kuondoa tatizo la ajira kwa vijana Afrika,” alisema Kimaro.

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Uzalishaji Mazao kutoka Wizara ya Kilimo, Justa Katunzi alisema ni muhimu Watanzania watumie mkutano huo kuonesha kahawa kwa kuwa ni sehemu ya kuongeza uchumi wa taifa.

Katunzi alisema ni muhimu vijana wakafahamu kwamba kahawa ni zao muhimu litakalosaidia kutatua changamoto ya ajira na kuimarisha uchumi wao.

Katibu Mkuu wa Shirika la Kahawa Afrika (IACO), Balozi Solomon Rutega alisema mkutano huo ni muhimu katika kuhakikisha nchi za Afrika zinanufaika na kahawa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Kahawa ya Amir Hamza Ltd, Amir Hamza amempongeza, Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu mkutano huo kufanyika nchini.

“Mkutano wa kwanza ulikuwa Kenya, wa pili Uganda na huu ni wa tatu nchini Tanzania, mkutano huu kufanyika hapa nchini ni manufaa makubwa sana kwetu kwani mambo mengi yatajadiliwa na kufikiwa mwafaka, mfano ajira kwa vijana, kahawa inatoa ajira nyingi kwa vijana wetu,” alisema Hamza.

Tanzania ni ya nne kwa uzalishaji wa kahawa baada ya Ethiopia inayoshika nafasi ya kwanza ikifuatiwa na Ivory Coast na Uganda.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *