WASHINGTON: WIZARA ya Sheria ya Marekani imewafungulia mashtaka raia wake wanne kwa tuhuma za kuhusika katika jaribio la kupindua Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kufuatia kurejeshwa kwa watatu kati yao mikononi mwa mamlaka za Marekani.
Raia ao, Marcel Malanga, Tyler Thompson, na Benjamin Zalman-Polun, walikuwa tayari wamehukumiwa nchini DRC kwa kushiriki katika jaribio hilo lililoshindikana Mei 2024, ambapo kundi lenye silaha lilivamia makazi ya viongozi wa serikali na kwa muda mfupi kuingia Ikulu jijini Kinshasa.
Kwa mujibu wa taarifa ya Marekani, raia hao wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama ya kutumia silaha za maangamizi, kutaka kulipua majengo ya serikali, na kupanga mauaji au utekaji nyara dhidi ya viongozi wa DRC.
“Walipanga mashambulizi kwa makusudi, wakawatambua waathiriwa waliolengwa, wakiwemo viongozi wa juu serikalini, na kuwahamasisha wengine kujiunga na mpango huo wa kijeshi,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha, inadaiwa kuwa walitoa malipo kwa baadhi ya watu ili kuwashawishi kujiunga na kundi hilo linalodaiwa kuwa la waasi. SOMA: Watu 7,000 wafa DR Congo
Washtakiwa hao watatu walikuwa miongoni mwa watu 37 waliopatikana na hatia Septemba mwaka jana na kuhukumiwa adhabu ya kifo kwa tuhuma za ugaidi na kula njama ya kupindua Serikali ya DRC.Hata hivyo, Rais wa DRC, Félix Tshisekedi, alibadilisha hukumu yao ya kifo kuwa kifungo cha maisha kabla ya kuwakabidhi kwa Marekani.
Taarifa zinaeleza kuwa hatua hiyo ilihusishwa na mazungumzo ya kidiplomasia kuhusu uwekezaji wa Marekani katika sekta ya madini ya DRC. Hapo awali washtakiwa hao watatu walikana mashtaka na walikata rufaa bila mafanikio.