Marekani kuiwekea vikwazo Afrika ya Kusini

MAREKANI: RAIS wa Marekani Donald Trump amesema atatimizia ahadi yake ya kuiadhibu Afrika Kusini kwa kusaini amri ya rais ya kusitisha misaada yote ya nchi yake kuelekea Afrika Kusini.
Utawala wa Trump umesema kuwa sheria ya umiliki wa ardhi ya Afrika Kusini iliyopitishwa hivi karibuni ni ubaguzi wa rangi dhidi ya jamii ya wazungu wenye asili ya Uholanzi na nchi nyingine za kikoloni za Ulaya.
Pia, utawala huo umeishutumu Afrika Kusini kuunga mkono kundi la wanamgambo wa Kipalestina la Hamas, Urusi, na Iran.
Ugawaji ardhi nchini Afrika Kusini umekuwa suala tata na lenye kuzua hisia za ubaguzi wa rangi kwa zaidi ya miaka 30 tangu kumalizika kwa utawala wa kibaguzi mwaka 1994.
Suala hili lilizua mjadala kimataifa baada ya Rais Trump na mshauri wake mzaliwa wa Afrika Kusini, Elon Musk, kukosoa sera za serikali ya Pretoria na kudai kuwa zinawabagua makaburu.
Sheria mpya ya usimamizi wa umiliki wa ardhi inatoa mamlaka kwa serikali ya Afrika Kusini kutaifisha ardhi kutoka kwa watu binafsi, lakini kwa masharti kwamba litakuwa ni kwa maslahi ya umma.
Hata hivyo, makundi yanayoipinga sheria hiyo nchini Afrika Kusini yanasisitiza kwamba hakuna ardhi ambayo imechukuliwa hadi sasa. SOMA: Rais Ramaphosa akubali yaishe kuhusu mzozo wa ardhi

Serikali ya Afrika Kusini inasema kuwa haki za mali za watu binafsi zinalindwa na kwamba taarifa zinazotolewa na Rais Trump kuhusu sheria hiyo ni za uongo na upotoshaji. Ingawa hivyo, sheria hiyo imezua wasiwasi nchini humo, hasa kwa makundi ya wazungu, ambao wanaamini kuwa wataathirika na kutaifishwa kwa ardhi yao.
Katika kipindi cha utawala wa ubaguzi wa rangi, ardhi ya watu weusi ilichukuliwa kwa nguvu na walilazimishwa kuishi katika maeneo yaliyotengwa mbali na wazungu. Leo hii, wazungu wanamiliki asilimia 70 ya mashamba binafsi nchini Afrika Kusini, ingawa ni asilimia 7 tu ya idadi ya watu, ambayo ni milioni 62.
Serikali ya Afrika Kusini inasema kuwa ukosefu huu wa usawa lazima ushughulikiwe.



