Rais Ramaphosa akubali yaishe kuhusu mzozo wa ardhi

AFRIKA YA KUSINI : RAIS wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, amechukua hatua ya kumaliza mzozo kati yake na utawala wa Marekani kuhusu sheria mpya ya ardhi kwa kuzungumza na mjasiriamali Elon Musk.
Musk, ambaye ni mshauri wa karibu wa Rais wa Marekani, Donald Trump, alielezea wasiwasi wake kuhusu sheria hiyo mpya, akitishia kusitisha ufadhili wa siku zijazo kwa Afrika Kusini kwa madai kuwa inanyakua ardhi na kudhulumu tabaka fulani la watu.
Bilionea huyo wa teknolojia, mzaliwa wa Afrika Kusini, alichapisha ukosoaji wake kupitia mtandao wa X, akijiuliza: “Kwa nini Ramaphosa ana sheria za wazi za ubaguzi wa rangi katika umiliki wa ardhi?”
Ofisi ya Rais Ramaphosa ilisema kuwa mazungumzo ya simu kati ya rais na Musk yalijikita katika kuhakikisha kuwa maadili ya Afrika Kusini, kama yalivyowekwa kikatiba, yanaheshimu utawala wa sheria, haki, na usawa.
Mwezi uliopita, Rais Ramaphosa alitia saini sheria inayoruhusu unyakuzi wa ardhi bila fidia kwa baadhi ya hali, hatua ambayo imezusha mjadala mkubwa nchini na kimataifa.
Umiliki wa ardhi umekuwa suala tete nchini Afrika Kusini, ambapo mashamba mengi ya binafsi bado yanamilikiwa na watu weupe, miaka 30 baada ya kumalizika kwa mfumo wa ubaguzi wa rangi.
Serikali ya Afrika Kusini imekuwa ikikumbwa na wito wa mara kwa mara wa kufanya mageuzi ya ardhi ili kukabiliana na dhuluma za zamani za ubaguzi wa rangi.
SOMA: Ramaphosa agoma kujiuzulu
Katika majibu yake kwa Rais Trump, Ramaphosa alisisitiza kuwa serikali yake haijamnyang’anya ardhi yoyote. Trump alijibu kupitia mtandao wake wa kijamii wa Truth Social, akisema: “Nitakata ufadhili wote wa siku zijazo kwa Afrika Kusini hadi uchunguzi kamili wa hali hii ukamilike!”
Sheria mpya ya Afrika Kusini inaruhusu unyakuzi wa ardhi bila fidia katika hali ambazo ni “haki na sawa kwa maslahi ya umma,” ikiwa ardhi haitumiki, haizalishi faida, au ikiwa inahatarisha usalama wa watu.
Historia ya utawala wa kikoloni wa Uingereza mwaka 1913 ilianzisha sheria iliyozuia haki ya kumiliki ardhi kwa watu weusi, ambao ni wengi nchini humo.
Sheria hiyo ilifanya sehemu kubwa ya ardhi kuwa chini ya udhibiti wa Wazungu wachache, huku watu weusi wakilazimishwa kuondolewa katika ardhi zao na kuhamishiwa katika vitongoji maskini kwa miongo kadhaa hadi kumalizika kwa ubaguzi wa rangi.



