‘Marekebisho ya sheria yataboresha ufanisi ‘

DODOMA; Wabunge wameipongeza Serikali kwa kuwasilisha bungeni marekebisho ya sheria kwa lengo la kuboresha ufanisi na kuendana na mabadiliko ya kiutendaji serikalini.

Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kuhusu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 3 wa Mwaka 2023, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Florent Laurent Kyombo, amesema kamati inaona ni muhimu kuhakikisha kuwa sheria zinakwenda sambamba na mabadiliko ya kiutendaji serikalini ili kuleta tija na ustawi kwa wananchi

Amesema wameuchambua muswada huo uliogawanyika katika sehemu kuu tatu na unapendekeza kufanya marekebisho katika sheria mbili kwa madhumuni ya kuondoa upungufu au kutatua changamoto, ambazo zimejitokeza katika utekelezaji wa sheria hizo.

“Kamati inaipongeza serikali kwa hatua hii ya kuleta marekebisho haya muhimu kwa lengo la kuboresha ufanisi na uendeshaji wa majukumu ya Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji.

Kamati inaona kuwa ni muhimu kuhakikisha kuwa sheria zetu zinakwenda sambamba na mabadiliko ya kiutendaji serikalini ili kuleta tija na ustawi kwa wananchi

“Kamati imeridhika kwamba, marekebisho yanayopendekezwa yatasaidia utekelezaji bora wa sheria zinazohusika na kwamba yamezingatia hati idhini ya mgawanyo wa majukumu ya Mawaziri ambayo hutolewa na Rais.

“Kwa sasa sheria hizi zinamtafsiri Waziri kama Waziri mwenye dhamana ya viwanda, ilihali jukumu la usimamizi wa masuala haya limehamishiwa Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji,” amesema Makamu Mwenyekiti.

Awali akiwasilisha muswada huo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Eliezer Feleshi ametaja sheria zinazopendekezwa kufanyiwa marekebisho ni Sheria ya Kanda Maalum za Uwekezaji kwa ajili ya Mauzo Nje ya Nchi, Sura 373 (The Export Processing Zones Act, (Cap. 373)); na (b) Sheria ya Kanda Maalum za Kiuchumi, Sura ya 420 (The Special Economic Zones Act, (Cap. 420). Bunge limejadili na kupitisha muswada huo.

Habari Zifananazo

Back to top button