Masauni aagiza uchunguzi polisi kusababisha kifo

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni ameagiza Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro kufanya uchunguzi wa kina kwa kushirikisha vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuhusu  askari wa Kituo cha Polisi Dakawa wanaodaiwa na wananchi kuhusika kumpiga Yassin Mangube (34), mkazi wa Dakawa na baadaye kusababisha kifo.

Masauni alitoa agizo hilo juzi wakati akijibu hoja zilizoibuliwa na wananchi wa Dakawa kwenye mkutano wa hadhara ambao uliandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Mvomero, Jonas Van Zeeland.

Kabla ya Waziri kutoa agizo hilo, Zeeland alimfahamisha Masauni kuhusu utendaji wa baadhi ya askari wa kituo hicho ambacho pia kinatumika kama Ofisi ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya na kwamba wanakiuka misingi ya haki, maadili na utaratibu unaopaswa kutumika wanapokamata mtuhumiwa kwa tuhuma mbalimbali.

Advertisement

Alieleza tukio mojawapo ni la kifo cha kutatanisha cha kijana Yassin ambaye inadaiwa alifariki dunia kutokana na  kipigo cha askari wa kituo hicho baada ya kukamatwa kwa kudaiwa kuchukua simu ya mama yake mdogo.

“Leo niseme wazi mbele yako Waziri, hapa Dakawa kuna changamoto kubwa sana ikiwemo ya yule kijana aliyepoteza maisha akiwa mikononi mwa polisi. Naomba kupitia vyombo vyako ikikupendeza uunde tume ichunguze ukweli ubainike juu ya huyu kijana aliyepoteza maisha kwa kudaiwa kupigwa na askari wa kituo hicho,” alisisitiza Mbunge huyo.

Kufuatia hoja ya mbunge huyo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima ambaye aliambatana na Masauni alisimama na kutoa nafasi kwa mlezi wa Yassin ambaye alikuwepo katika mkutano huo kuelezea kwa kina jambo hilo.

Mlezi wa Yassin, Tabu John aliposimama alisema yeye ndiye aliyemlea marehemu na kwamba kabla ya kukamatwa siku hiyo alipita nyumbani kwake na alimtuma kununua unga dukani.

Mama huyo mlezi alisema chanzo cha tukio hilo ni kwamba Yassin alikuwa akimdai mama yake mdogo simu na kuamua kuchukua simu anayomiliki mama yake huyo kwa lengo la kumshinikiza arudishe simu yake.

Alisema muda mfupi baada ya kuichukua simu ya mama yake mdogo, askari wa kituo hicho cha Dakawa walifika  nyumbani hapo na kumtia mbaroni kisha kumfikisha kituoni.

“Ilipita muda wa saa moja ama mawili kijana Yassin amerudi nyumbani akiwa anatema damu na aliniamsha wakati nikiwa nimelala na kuniambia mimi ‘Yassin’ nimepigwa na kuwataja polisi waliompiga na ilipofika asubuhi hali yake ilibadilika na kupelekwa hospitali na mimi (Tabu) nilienda kwenye kikao lakini baadaye napigiwa simu na kuambiwa kuwa Yassin amefariki wakati zilipita saa tatu nilipokuwa naye, lakini bado askari hao wapo tu mpaka leo,” alisisitiza Tabu.

Akijibu tuhuma hizo baada ya kutakiwa na Waziri, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro, Hassan Omary alikiri kutokea kwa tukio hilo Juni 3, 2023 na ilidaiwa mtuhumiwa alienda kumfanyia fujo mama yake mdogo.

Omary alisema baadaye alikamatwa na askari na kufikishwa kituoni hapo na baada ya muda mfupi hali yake ilibadilika na kufikishwa katika zahanati kwa ajili ya matibabu lakini umauti ulimfika.

Alisema baada ya kufariki jalada lilifunguliwa dhidi ya askari na walishikiliwa kama watu wengine.

Omary alisema kuwa uchunguzi wa mwili ulifanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro na kuletwa mtaalamu kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili na ulifanyika mbele ya ndugu wa marehemu.

Aliongeza kuwa matokeo ya uchunguzi yalionesha kuwa kifo chake hakitokani na kipigo bali ni jambo lingine na jalada la kesi lilipelekwa Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali ndiye mwenye Mamlaka ya kupeleka mahakamani ama laa.

“Jalada lilifikishwa kwa Mwanasheria wa Serikali na wao waliona hakuna ushahidi wa kuwafikisha askari hawa mahakamani na mimi ninachokiona ni changamoto ya mawasiliano kati yetu sisi  polisi mkoa na Ofisi ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,” alisema Kaimu Kamanda Omary.

Baada ya hoja hiyo, Masauni alisema bado tukio hilo lina ukakasi ndani yake na kuagiza uchunguzi.

Aliwataka wananchi wenye ushahidi zaidi wajitokeze kuuwasilisha kwenye vyombo shirikishi kwa vile kesi ya jinai haina mwisho kwa kuwa suala hilo bado halijafikishwa mahakamani hivyo uchunguzi zaidi unaweza kuendelea.

“Nakuomba Mbunge na wananchi mshirikiane kusimamia hili uchunguzi ufanyike hadi pale wananchi watakaporidhika,” alisema Masauni.

1 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *