Mashirika 15 ya umma yanajiendesha kwa mikopo

DODOMA — Ripoti Kuu ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2023/2024 imebainisha kuwa mashirika 15 ya umma yanajiendesha kwa kutegemea mikopo kwa zaidi ya asilimia 100 ya mtaji wao.
Hali hii inaashiria kuwa mashirika hayo hayawezi kujiendesha bila kukopa, hivyo kuyaweka kwenye hatari kubwa ya kifedha.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, baadhi ya mashirika yamefikia viwango vya kutisha vya utegemezi wa mikopo, huku Kampuni ya Ushauri Elekezi wa Mazingira ya Chuo Kikuu Ardhi ikiongoza kwa uwiano wa asilimia 1137.
Hii ina maana kuwa kwa kila shilingi moja ya mtaji, kampuni hiyo inategemea zaidi ya shilingi kumi na moja za mkopo. Mashirika mengine yaliyoorodheshwa ni pamoja na Soko la Bidhaa Tanzania (asilimia 379), Kituo cha Uwekezaji Tanzania (APC) (asilimia 266), na Mamlaka ya Bandari Tanzania (asilimia 248).
“Uwiano huu wa mikopo na mtaji ni ishara ya hatari ya kifedha, hasa wakati wa misukosuko ya kiuchumi au kushuka kwa soko,” imeonya ripoti hiyo, ikisisitiza kuwa mashirika haya yanaweza kushindwa kutimiza majukumu yake ya msingi endapo masharti ya mikopo yatabadilika au mapato yatashuka ghafla.
Mbali na hilo, ripoti imeonesha kuwa baadhi ya mashirika yanakumbwa na athari za gharama kubwa za mikopo, hasa kutokana na ucheleweshaji wa malipo ya riba na deni kuu. Miongoni mwao ni Kiwanda cha Dawa cha Keko, Kampuni ya Gesi Tanzania, na Kampuni ya STAMIGOLD, ambazo zote zina uwiano hasi unaoonesha matumizi ya mikopo kupita kiasi.
CAG amependekeza mashirika husika kuimarisha usimamizi wa fedha, kutathmini upya muundo wa mtaji na kupunguza utegemezi wa mikopo. Vilevile, ameiomba Serikali kufanya tathmini ya uwepo wa mashirika haya na kuangalia uwezekano wa kuunganisha, kubinafsisha, au kufuta baadhi yao ili kupunguza mzigo wa kifedha kwa taifa.
“Lazima Serikali itathmini uwepo wa haya mashirika na kuangalia kama inahitaji kuendelea nayo au la,” amesema CAG katika hitimisho la ripoti hiyo.



