Mashujaa FC: Tunataka nafasi nne za juu

SIKU chache baada ya uongozi wa timu ya Mashujaa FC kutangaza benchi jipya la ufundi kufuatia kumtimua kocha wake, Mohamed Barres wachezaji wa timu hiyo wamesema wanaamini malengo yao ya kuifanya timu hiyo kushika nafasi ya nne za juu katika msimamo wa Ligi Kuu yako pale pale.
Wakizungumza na waandishi wa habari wachezaji wa timu hiyo walisema kuwa wanaamini kocha mpya aliyetangazwa na uongozi wa timu hiyo Salum Mayanga anayo nafasi yake katika kutimiza malengo hayo.

Mmoja wa wachezaji hao Luben Lyanga amesema ujio wa kocha huyo ni jambo la kawaida kwa uongozi unapoona ipo sababu ya kufanya hivyo hasa katika kupata matokeo hivyo wanampokea kocha kwa mikono miwili na watafanya naye kazi kulingana na mpango kazi wake na falsafa aliyokuja nayo.
Naye Mshambuliaji Mohamed Mussa amesema kuwa mabadiliko ya uongozi katika benchi la ufundi ni kawaida na bahati mbaya wamefanya vibaya hadi sasa kwenye msimamo wa ligi lakini baada ya mapumziko ya mechi za Timu za Taifa wanarudi na nguvu mpya na ari mpya na kila watakayekutana naye sasa ni fainali.
Kwa upande wake mshambuliaji Chrispin Ngushi amesema kuwa mechi ya kwanza ambayo wanataka kuirudisha timu kwenye nafasi yake ni mechi dhidi ya Pamba Jiji kwenye mashindano ya kombe la Shirikisho mechi itakayopigwa uwanja wa Lake Tanganyika jumamosi Machi 29 mwaka huu ambapo wanaamini ushindi watakaopata ndiyo utapeleka morali kubwa kwenye ligi kuu.

Kocha Salum Mayanga akizungumzia nafasi yake kwa timu ya Mashujaa amesema kuwa anafarijika kukuta timu ina vijana wenye ari ambao wako tayari kupambana na atafanya awezalo kuhakikisha timu inarudi na kufanya vizuri kwenye mechi za ligi lakini pia mechi yao ya kombe la Shirikisho na Pamba na Jiji.
Mayanga amesema kuwa nafasi ya timu iliyopo sasa ni dhahiri ilikuwa na ukame wa kufunga magoli hivyo ataanza na hilo kuwanua washambuliaji vilivyo lakini pia kuhakikisha nafasi ya ulinzi inakuwa imara isiweze kuruhusu mabao kirahisi ambapo alisema kuwa mchezo wa mechi ya Shirikishi na timu ya Pamba jiji itakuwa ndiyo kipimo kuelekea kwenye mafanikio ya ligi.



