Matamanio ya Rais Samia yanavyotimia kupitia ‘M300’

Rais Samia akiwa na wakuu wa nchi za Afrika waliohudhuria Mkutano wa Nishati wa ‘M300’ uliofanyika Dar es Salaam hivi karibuni.

KWA muda mrefu Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akitamani nchi za Afrika ziungane kufanya jambo la pamoja, katika kuwapunguazia wananchi gharama za maisha na kuwapa maendeleo yanayoendana na kasi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia matumizi ya nishati salama ya kupikia.

Mwaka 2023 akiwa Marrakesh, Morocco kwenye kongamano la siku mbili kuhusu masuala ya uwekezaji kwa nchi za Afrika, Rais Samia alitaka viongozi wa Afrika kufikiria namna ya kuliunganisha bara hilo kwa miundombinu huku akisisitiza amani na demokrasia imara.

Ni nguvu hiyo hiyo Rais Samia amekuwa akiitumia kushawishi mataifa ya Afrika kuungana ili kutafuta suluhu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kuikoa Afrika na matukio ya hali mbaya ya hewa.

Advertisement

Rais Samia amekuwa kinara wa kampeni ya matumizi ya nishati safi ya kupikia akihamasisha matumizi hayo ndani na nje ya Tanzania, akiwashawishi viongozi wenzake wa Afrika kushikilia kampeni hiyo kwa manufaa ya vizazi vijavyo vya Afrika, lakini akishinikiza pia mataifa yaliyoendelea kutimiza ahadi zao walizoziweka kupitia mkataba wa
Paris wa mabadiliko ya tabia nchi.

Siku zote ametamani kuona Afrika na mabara mengine yanaungana kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia matumizi ya nishati salama ikiwemo gesi na umeme. Hatimaye! Ndoto ya Rais Samia inaonekana kutimia
baada ya wakuu wa nchi 25 za Afrika kukutana na kujadili namna ya kuwafikishia umeme waafrika wengi zaidi.

Januari 28 na 29, Tanzania ilipata ugeni mkubwa wa wageni zaidi ya 85 wakiwemo marais 25 kutoka nchi mbalimbali za Afrika waliofika kuhudhuria mkutano wa nishati wa Misheni 300.

Katika mkutano huo, nchi 12 zilisaini Azimio la Dar es Salaam lenye lengo la kuhakikisha wananchi milioni 300 Afrika wanapata nishati ya umeme ifikapo mwaka 2030. Nchi zilizosaini azimio hilo ni Tanzania, Chad, Ivory
Coast, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Liberia, Madagascar, Malawi, Mauritania, Nigeria, Zambia,
Niger na Senegal.

Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Profesa Vincent Nmehielle aliyesoma azimio hilo, kwenye vipengele 15 viongozi hao wamedhamiria kuhakikisha wananchi milioni 300 katika mataifa hayo wanapata umeme na nishati safi ya kupikia kwa gharama nafuu na endelevu.

Alisema, viongozi hao wamekubaliana kuwe na mifumo shindanishi ya manunuzi ya umeme na kuwavutia wazabuni wenye uwezo. Ni katika Azimio hilo ndipo Rais Samia alipotangaza neema ya umeme akisema ili kutekeleza mpango huo nchi inahitaji uwekezaji wa Dola za Marekani bilioni 13 (Sh trilioni 33).

Alisema kati ya fedha hizo sekta binafsi inatarajiwa kutoa Dola za Marekani bilioni tano. Alisema mpango huo
mahususi wa kitaifa kuhusu nishati utatekelezwa katika mambo manne na utaongeza kasi kuunganisha umeme nchini hadi kufikia asilimia 72 ifikapo mwaka 2030.

“Ili kufanikisha azma hiyo ndani ya miaka mitano ijayo tutahitaji uwekezaji wenye thamani ya Dola za Marekani
bilioni 13 ambapo Dola bilioni tano zitapatikana kutoka sekta binafsi hapa nchini,” alisema.

Alisema sekta ya umma inahitaji uwekezaji wa Dola za Marekani bilioni 8.85 na kati ya fedha hizo Dola bilioni 2.062 ni uwekezaji wa miradi ya kuzalisha umeme.

Alisema miradi ya kusafirisha umeme inahitaji Dola za Marekani milioni 583.81 huku miradi ya kusambaza umeme ikihitaji Dola za Marekani milioni 550, ukarabati wa  miundombinu ya umeme Dola za Marekani milioni 398, miradi ya nishati safi Dola za Marekani milioni 400 huku Dola za Marekani milioni 647 zikihitajika kwa ajili ya kuwajengea uwezo wahusika wa utekelezaji wa mpango huo.

Alisema kupitia mpango huo Tanzania imepanga kutekeleza mambo makubwa manne ikiwa ni pamoja na kuongeza uzalishaji wa umeme kutokana na nishati mchanganyiko. “Hadi sasa Tanzania ina uwezo wa kuzalisha megawati 3,431 ambapo asilimia 58 ya hizo inatokana na vyanzo vya maji, asilimia 35 gesi na asilimia saba inatokana na vyanzo vingine,” alisema Rais Samia.

Alisema Tanzania imepanga kuongeza uzalishaji wa umeme wa megawati 2,463 kutoka vyanzo vingine kama jua, gesi asilia, upepo na vingine ifikapo 2030. Aidha, alisema kijiografia Tanzania ni kiungo muhimu cha kuunganisha nchi nyingine za Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika kwa nishati ya umeme na hivyo kutoa fursa ya biashara ya
nishati hiyo kutoka Afrika Kusini hadi Cairo, Misri.

“Tumeshaunganisha miundombinu ya umeme na nchi za Burundi, Rwanda, Kenya na sasa tunaendelea kuunganisha umeme na nchi ya Zambia na Uganda,” alisema Rais Samia.

Alisema uwepo wa miundombinu hiyo utawezesha biashara ya nishati kati ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika. Wachambuzi mbalimbali wa masuala ya uchumi na wadau wa nishati wametoa maoni yao wakiitabiria Tanzania kufika mbali kwenye biashara hiyo ya nishati ya umeme na hivyo kukuza
uchumi wa nchi na wananchi.

Mchambuzi wa masuala ya uchumi Walter Nguma alisema Azimio hilo lina faida kubwa kwa Tanzania kwani ni moja ya nchi za Afrika zinazofanya vizuri kwenye nishati ya umeme. “Tuna zaidi ya megawati 3,000 lakini kwa matumizi ya Tanzania ni takribani megawati 1,800 hivi kwa hiyo tuna umeme wa ziada kuuza nje hii itatusaidia kupata nafuu
ya umeme kwani tukiuza vizuri itatuletea mapato,” alisema.

Kuhusu mpango wa Rais Samia Suluhu Hassan kutumia Sh trilioni 33 kuwekeza kwenye umeme, Nguma alisema, “Usione vyaelea vimeundwa… hii ndio maana yake, tunataka biashara ya umeme lazima tuwekeze nina hakika Rais
amepata ushauri mzuri ndio maana ameingia kuwekeza, wote walioendelea kwenye biashara hii waliwekeza na
Rais anawekeza sasa kupanga ni kuchagua, kama fursa imeonekana kwenye nishati hakuna budi kuitumia.”

Aidha, alisema kama Azimio hilo na yote yaliyokubaliwa kwenye mkutano huo yatafanyika, Tanzania itapiga hatua kubwa kwenye uchumi wa nchi na watu wake. Alisema nishati ya umeme itakapokuwa ya kutosha Tanzania na Afrika bara hilo litakuwa na viwanda vya uhakika na watu wake watapata ajira.

Profesa Haji Semboja ambaye ni mtaalamu wa masuala ya uchumi na fedha kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema: “Tanzania itanufaika sababu sisi wenyewe ndio waafrika pia dunia inataka tubadilike Afrika tutumie nishati kwa maendeleo, iwekwe mipango mikakati mizuri ya kututoa tulipo na kusonga mbele.”

1 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *