Matapeli 11 wadakwa na laini 9,389 za simu

JESHI la Polisi Mkoa wa Geita linawashikilia watu 11 kwa tuhuma za kukutwa na laini 9,389 za mitandao ya simu walizokuwa wakitumia kufanyia matukio mbalimbali ya uharifu kwa njia ya mtandao na unyang’anyi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Kamishina Msaidizi wa Polisi (SACP) Safia Jongo ametoa taarifa hiyo  kwa waandishi wa habari mjini Geita.

Watuhumiwa hao ni Ilege Charles (42), Shabani Abdallah (25), Daudi Omary (25), Alex Rashid (32), Jumanne Mageso (27), Meshack Bahebe (31), Alex Edward (29), Nkwabi Ipilinga (21), Dennis Ndihunze (33), Vicent Vedastus (25) na Hamduni Issa (30).

Amesema watuhumiwa walikutwa na vifaa vingine vya kufanyia uharifu ikiwemo Laptop moja aina ya HP, Mashine mbili za kusajili line kwa kutumia alama za vidole, imu janja (Smartphone) 15.

“Pia kuna simu ndogo za kawaida 18, laini  mpya za mitandao mbalimbali 1,600, Mabaki ya laini za mitandao mbalimbali jumla 6189, Line za Yass (Tigo) zilizosajiliwa 2600 na begi tatu za mgongoni”, ameeleza Kamanda.

Amebainisha watuhumiwa walikamatwa Machi 13, 2025 katika Kata ya Ludete, wilayani Geita baada ya Jeshi la Polisi kupata taarifa juu ya uwepo wa wahalifu hao na kuweka mtego uliofanikisha kuwakamata.

Ameeleza Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kwa kushirikiana na taasisi nyingine ili kuweza kubaini mtandao mzima wa wahalifu hao ili kuwadhibiti na kuwachukulia hatua kali za kisheria.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button