IMEPENDEKEZWA matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na utendaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuhojiwa mahakama ya juu mara itakapoanzishwa ili kuongeza uwajibikaji wa tume hiyo.
Mapendekezo hayo ni miongoni mwa yaliyotajwa na Kikosi Kazi cha kuratibu maoni ya wadau wa demokrasia ya vyama vingi ambacho kilikabidhi ripoti yake kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu Dar es Salaam jana.
Mwenyekiti wa Kikosi Kazi hicho, Profesa Rwekaza Mukandala, alisema mapendekezo mengine ni kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi haipaswi kulazimika kufuata amri au maagizo ya mtu yeyote, idara yoyote ya serikali, maoni ya chama chochote cha siasa, taasisi au asasi yoyote katika shughuli zake.
Kikosi kimependekeza pia kuwapo kwa kamati ya uteuzi wa wajumbe wa tume hiyo ya taifa ya uchaguzi itakayokuwa na wajumbe mbalimbali akiwamo Jaji Mkuu wa Tanzania ambaye atakuwa mwenyekiti.
Wajumbe wengine ni Jaji Mkuu wa Zanzibar atakayekuwa Makamu Mwenyekiti, Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya Tanzania Bara na Mwenyekiti wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya Zanzibar.
Aliwataja wajumbe wengine wanaopaswa kuwamo kwenye kamati hiyo ni pamoja na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na wajumbe wawili watakaoteuliwa na Jaji Mkuu, baada ya kupendekezwa na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na Chama cha Wanasheria Zanzibar.
“Angalau wajumbe wawili wa kamati ya uteuzi wawe wanawake, nafasi ya mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi itangazwe na Mtanzania yeyote mwenye sifa aruhusiwe kuwasilisha maombi kwa kamati ya uteuzi ya kuwa mjumbe wa tume,” alisema Profesa Mukandala.
Vilevile imependekezwa kamati ya uteuzi kuwa na jukumu la kufanya usaili wa watu waliowasilisha maombi ya kuwa wajumbe wa tume na kupendekeza kwa Rais majina ya watu wanaostahili kuteuliwa kuwa wajumbe wa tume.
Pendekezo jingine ambalo kikosi kililiwasilisha ni kwa kamati ya uteuzi kuwasilisha kwa Rais majina manne zaidi ya idadi ya nafasi zinazohitajika kujazwa na Rais atateua wajumbe wa tume miongoni mwa majina yaliyowasilishwa kwake na kamati ya uteuzi.
Kikosi Kazi kimependekeza watendaji wa tume, yaani wasimamizi wa uchaguzi, wazingatie sheria, weledi, maadili, uwazi na ushirikishwaji wa wadau wakati wa kufanya kazi zao na wasimamizi watakaokiuka sheria na utaratibu wawajibishwe kwa mujibu wa sheria.
Mapendekezo mengine ni kwamba tume ipewe fedha zilizotengwa katika bajeti kwa wakati hata baada ya uchaguzi kuiwezesha kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi wakati wote.
“Kuhusu sheria zinazosimamia masuala ya uchaguzi, kikosi kazi kinapendekeza kuwa itungwe sheria ya kusimamia shughuli za Tume ya Taifa ya Uchaguzi, kuwepo sheria moja ya uchaguzi itakayosimamia uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani,” alisema Profesa Mukandala.