MATUKIO MAKUBWA MWAKA 2024: Kanisa la Anglikana laomba msamaha

Zanzibar

MEI mwaka huu Kanisa la Anglikana liliomba radhi kwa Kanisa la Tanzania kwa makosa liliyowafanyia watu wa Zanzibar wakati wa biashara ya utumwa.

Aliyekuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Duniani, Justin Welby aliomba msamaha huo wakati wa Misa ya Upatanisho katika Kanisa Kuu la Mkunazini, Unguja.

“Nakuja mbele zako na natubu kwa niaba ya Kanisa la Uingereza kwa makosa tuliyowafanyia na tunaomba msamaha, namuomba Mungu baraka zake ili tuweze kufanya vizuri siku zijazo,” alisema Askofu Mkuu Welby.

Advertisement

Alisema Waingereza walitambua ulimwengu unatakiwa kubadilika kupitia nguvu za Yesu Kristo ndio maana waliamua kujenga kanisa kuu ili kupambana na utumwa lakini hilo halikukamilisha toba, hivyo ilikuwa muhimu kutubu.

Askofu Mkuu Welby alisema wametenga paundi milioni 100 kuwekeza katika kuwanufaisha waathirika wa utumwa ili nao wawe na maisha mazuri ya baadaye.

Alisema jambo hilo limekuwa na vipingamizi na amepokea vitisho kutokana na hilo kwa kuonekana kuwa anaisaliti nchi yake.

“Tumesikia maktaba ya Oxford ina nyaraka za urithi wenu na vilevile maktaba ya Lamberth, nimesikiliza na nitauliza swali kuhusu Zanzibar bungeni na kuzungumza na Mkuu wa Chuo cha Oxford, tutangalia katika maktaba yangu na kufanya niwezacho kueleza tunatakiwa kutubu na kuangalia kile tulichokifanya,” alisema Askofu Mkuu Welby.

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi alisema Kanisa la Anglikana limefanya jambo la aina yake kutubu na kuomba msamaha na amelishukuru kwa uungwana.

“Kwa hulka ya binadamu kukiri makosa ni jambo gumu sana, wamekiri makosa, lakini vilevile wameomba msamaha. Tuchukue fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza kwa jambo hili, tumuombe Mwenyezi Mungu awasamehe, na sisi yaliyotukuta haya tuwe tayari kusamehe,” alisema Dk Mwinyi.

Awali, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Maimbo Mndolwa alisema mwaka jana Rais wa Ujerumani wakati wa ziara nchini aliomba radhi kwa Watanzania.

Askofu Mkuu Mndolwa alisema kwa kuwa Uingereza haijawahi kufanya hivyo alimuomba Askofu Mkuu Welby aseme neno kwa Watanzania.

Vilevile alisema kwa kuwa Kanisa la Uingereza linafanya ukaguzi wa hesabu wa fedha zilizopatikana kutokana na biashara ya utumwa alimuomba Zanzibar ijumuishwe katika hesabu hizo.

Wakati wa Misa hiyo Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi alilisamehe Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Zanzibar kwa kutolipa kodi kutokana na mapato ya utalii.

Awali Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Maimbo Mndolwa aliomba serikali iwasamehe kwa kuwa Kanisa Kuu la Kristo Mkunazini linapata fedha nyingi kupitia malipo ya utalii lakini halijawahi kulipa kodi.

“Kwa kuwa tumeiba vya kutosha na kwa kuwa hatuwezi kurudisha tulichoiba, nitumie fursa hii kumuomba Rais wa Zanzibar ukiona vyema tutamkie tu kutusamehe ndugu yangu,” alisema.

Dk Mwinyi aliagiza uwekwe utaratibu mzuri wa makusanyo ili serikali ipate sehemu yake na kanisa lipate sehemu yake.

Aidha, alisema amekubali ombi la kanisa kwamba Juni 6, kila mwaka kuwe na maadhimisho ya kukumbuka kusitishwa kwa biashara ya utumwa.

Imeandikwa na Lidya Inda na Prisca Pances.