MATUKIO MAKUBWA YA MWAKA 2024: Kwaheri Mzee Rukhsa, Lowassa

MWAKA 2024, Tanzania imepoteza viongozi na watu mashuhuri walioacha alama kubwa katika historia ya taifa.
Miongoni mwao ni Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi, ambaye alifariki dunia tarehe Februari 29, 2024. Kifo chake kilitangazwa na Rais wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan.
Mwinyi maarufu kwa jina la Mzee Rukhsa, alikuwa kiongozi muhimu katika siasa za Tanzania, akiwa Rais wa Awamu ya Pili wa kuanzia mwaka 1985 hadi 1995.
Kabla ya kuwa Rais wa Tanzania, Mwinyi alihudumu kama Rais wa muda wa Zanzibar na Makamu wa Pili wa Rais wa Tanzania.
Alijiunga na chama cha Afro Shiraz Party (ASP) mwaka 1964, ambapo alishika nyadhifa mbalimbali serikalini, ikiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Zanzibar mwaka 1963, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1970, na Waziri wa Afya kati ya 1982 na 1983.
Mwinyi pia alihudumu kama Waziri wa Mambo ya Ndani, Waziri wa Maliasili, na Balozi wa Tanzania nchini Misri. SOMA: Mwinyi ndiye alianzisha neno unyanyapaa
Katika kipindi cha uongozi wake, alileta mageuzi makubwa ya kiuchumi, hasa baada ya vita vya Kagera.
Alianzisha sera zinazovutia uwekezaji wa kigeni, jambo lililochangia kuimarika kwa uchumi wa taifa na kupanuka kwa sekta za kilimo, viwanda, na huduma za kifedha. Mwinyi atakumbukwa kama kiongozi aliyechangia sana katika mabadiliko ya uchumi wa Tanzania na mafanikio ya kitaifa.
Hayati Edward Lowassa
Kiongozi mwingine mashuhuri aliyefariki mwaka huu nii Edward Lowassa, aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania.
Lowassa alifariki dunia Januari 14, 2024, akipatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, jijini Dar es Salaam, baada ya kuugua kwa muda mrefu. Kifo chake kilitangazwa na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango.
Lowassa alihudumu kama Waziri Mkuu wa Tanzania kuanzia mwaka 2005 hadi 2008, chini ya Rais Jakaya Kikwete, kabla ya kujiuzulu kufuatia kashfa ya Richmond.
Mwaka 2015, alihama chama tawala cha CCM na kujiunga na chama cha upinzani cha Chadema, akagombea urais kwa kupokea msaada kutoka kwa vyama vya upinzani vya UKAWA. Hata hivyo, alishindwa na Dk John Magufuli, mgombea wa CCM. Alirejea CCM mwaka 2019.
Lowassa, ambaye alizaliwa Agosti 26, 1953, alifariki akiwa na umri wa miaka 70, atakumbukwa kama mmoja wa miamba ya siasa za Tanzania. Rais Samia Suluhu Hassan alielezea huzuni yake akisema, “Tumepoteza kiongozi mahiri, aliyejituma na kujitoa kwa nchi yetu.”
Mfanyabiashara Mustafa Sabodo
Mtu mwingine mashuhuri aliyefariki mwaka huu ni Mustafa Sabodo, ambaye alifariki dunia Machi 23, 2024.Sabodo alizaliwa mkoani Lindi, na alijipatia umaarufu mkubwa katika biashara.
Alikumbukwa hasa kwa mchango wake wa uzalendo, akiwemo kusaidia taifa wakati wa uhaba wa mafuta miaka ya 1970. Alimuomba Mwalimu Nyerere idhini ya kwenda Iran kuleta mafuta kwa ajili ya nchi.
Sabodo pia alikumbukwa kwa udhamini wake mkubwa kwa vyama vya siasa, ikiwemo Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).