Matukio: Tanzania yawa mwenyeji miaka 20 Baraza la Amani, Usalama AU

DAR ES SALAAM; MIONGONI mwa matukio makubwa ya kihistoria nchini kwa mwaka 2024 ni kuwa mwenyeji wa maadhimisho ya miaka 20 ya Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika (AU).

Ujumbe wa wageni 120, wakiwamo marais wastaafu wa nchi mbalimbali Afrika, walihudhuria maadhimisho hayo kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) Dar es Salaam.

Baraza la Amani na Usalama ni chombo cha juu cha uamuzi kuhusu masuala ya amani na usalama kwenye Umoja wa Afrika. Miongoni mwa majukumu ya baraza hilo ni kuzuia kutokea kwa migogoro, kusuluhisha au kukabiliana nayo pale inapojitokeza.

Baraza hilo lilianzishwa mwaka 2004 kuchukua nafasi ya Chombo cha Kuzuia na Kukabiliana na Migogoro cha uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU).

Mbali na kuwa mwenyeji wa maadhimisho hayo, Rais Samia Suluhu Hassan ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa baraza hilo kwa wakati huo Mei mwaka huu.

Tanzania ilichaguliwa kuwa Mjumbe wa baraza hilo Machi 2022 na kuhudumu kwa miaka miwili na kufikia ukomo Machi 2024, kabla ya kuchaguliwa tena katika Mkutano wa 37 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa AU uliofanyika Februari 2024 Adiss Ababa, Ethiopia na sasa itahudumu kwenye nafasi hiyo mpaka mwaka 2026.

Katika maadhimisho hayo, Rais Samia alisema dhamira ya Tanzania ni kukuza na kudumisha amani Afrika ili kujenga mazingira rafiki na ustawi wa kiuchumi kwa watu wote.

“Kama ilivyokuwa tangu enzi za Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, napenda kuwahakikishia kwamba Tanzania itaendelea kutoa kipaumbele katika kuhakikisha kuwa umoja wetu unafikia malengo tuliyojiwekea,” alisema Rais Samia.

Rais Samia alisema historia ya mafanikio ya Afrika katika harakati za ukombozi lazima iwape hamasa katika jitihada za sasa za kulinda amani, kujiletea maendeleo na kuhakikisha ustawi wa watu wao.

Alisema kaulimbiu ya maadhimisho hayo ‘Miaka 20 ya Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika kama chombo cha kudumu cha maamuzi, miongo miwili ijayo ya amani na usalama wa Afrika tuitakayo,’ inawataka Waafrika kujitafakari tangu kuanzishwa kwa baraza hilo (mwaka 2004) hadi sasa katika miongo miwili ya uwepo wake wamejifunza nini ili kuwa na Afrika wanayoitaka.

“Tangu kuanzishwa kwake Baraza la Amani na Usalama limekuwa na nafasi kubwa katika kukuza amani, usalama na utulivu katika bara letu la Afrika,” alisema.

Alisema tangu kuanzishwa kwa baraza hilo kumekuwa na mafanikio makubwa ikiwamo kukuza amani, usalama na utulivu Afrika na kutoa mchango mkubwa katika kukabiliana na migogoro na matishio mbalimbali ya kiusalama na ugaidi.

“Hata hivyo, bado kuna changamoto zinazohitajika kufanyiwa kazi hatujanyamazisha mitutu, uwepo wa uongozi usiofuata katiba, je tunafuata misingi yetu? Mimi sina majibu,” alisema Rais Samia.

Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete alikuwa miongoni mwa wageni waliohudhuria hafla hiyo na kueleza kuwa vyanzo vya migogoro kwenye nchi nyingi za Afrika ni kuhusiana na uongozi kukosa demokrasia na kutoaminiana.

“Viongozi kutoaminiana kunafanya wananchi pia kukosa imani nao, lakini pia chanzo kingine ni chaguzi ambazo mshindi anatangazwa mshindwa na mshindwa anatangazwa mshindi na kuanza migogoro ambayo pia huingia ukabila na watu kukosa haki zao,” alisema Kikwete.

Kwa upande wake, Rais mstaafu wa Nigeria, Olusegun Obasanjo aliunga mkono kauli ya Kikwete kuhusu chanzo cha migogoro Afrika akitolea mfano wa Libya na kutaka masuala ya Afrika yatatuliwe na waafrika wenyewe.

“Libya waliingia kwenye mgogoro na walituondolea jukumu letu na yaliyotokea nyote mliona,” alisema Obasanjo.

Naye Rais wa zamani wa Burundi, Domitien Ndayizeye alielezea namna ilivyokuwa ngumu kumaliza mgogoro wake na Rais wa zamani wa nchi hiyo, Pierre Buyoya.

Nchi 15 kati ya nchi 55 wanachama wa AU ndio wajumbe wanaounda baraza hilo.

Kwa sasa nchi hizo 15 ni Tanzania, Uganda na Djibouti (Ukanda wa Mashariki), Cameroon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Equatorial Guinea (Kati), Afrika Kusini, Angola na Botswana (Kusini), Ivory Coast, Gambia, Nigeria na Sierra Leone (Magharibi) na Misri na Morocco (Kaskazini).

 

Habari Zifananazo

Back to top button