Matuta 10 yawasubiri wachelewaji shuleni

DODOMA: MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema wanafunzi watakaochelewa kuripoti kidato cha kwanza watapata adhabu ya kulima matuta 10 ya viazi na kuwataka wazazi mkoani Dodoma kuhakikisha watoto wanaripoti shule na kuanza masomo kwa wakati.

Alisema hayo juzi alipotembelea na kukagua miradi ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Michese. Vilevile alisikiliza na kutatua kero za wananchi wa eneo la Michezo katika Kata ya Mkonze kwenye Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Akizungumza na wananchi wa Michese, Senyamule alisema mtoto atakayechelewa kuanza masomo kwa wakati atalima matuta 10.

Advertisement

“Wazazi msiwasababishie watoto adhabu ya kulima matuta 10 kwa sababu ya kuchelewa kufika shule kwa wakati na kuchelewa kuanza masomo wanafunzi wanaanza kusoma tangu siku ya kwanza wanapofungua shule,” alisema.

“Dodoma tunataka ufaulu wa kiwango cha juu kama ilivyo hadhi ya makao makuu ya nchi yetu tunaendelea kufanya vizuri kwenye masomo na hatutaki kurudi nyuma,” alisema.

Pia Senyamule alikagua ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Michese unaotekelezwa katika Kata ya Mkonze eneo la Michese na kuagiza kukamilika kwa wakati.

Kwa upande wake, Kaimu Ofisa Elimu wa Mkoa wa Dodoma, Justin Machela aliwataka wazazi kuwapeleka watoto wao shule na kuepuka malalamiko yasiyo na msingi ili kuhakikisha watoto wanaanza masomo kwa wakati. Alisisitiza wanafunzi wanunuliwe vifaa vinavyohitajika shuleni.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Mkonze, Andrew Rumishaeli alisema walipokea Sh milioni 544 ikiwa ni fedha za Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (Sequip) kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vinane vya madarasa vyenye ofisi mbili, jengo la utawala, jengo la maktaba, jengo la Tehama, vyoo vya wanafunzi matundu manane, kichomea taka na tangi la maji la ardhini.