Mauzo nyama nje ya nchi yafikia tani 14,000

SIMIYU: SERIKALI imesema kiwango cha kuuza nyama nje ya nchi kimeongezeka kutoka tani 1,000 hapo awali hadi 14,000 mwaka 2025.
Akizungumza na HabariLEO mapema leo Juni 16, 2025 katika mahojiano maalum, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Ashatu Kijajii amedokeza kuwa kwa sasa soko kubwa la bidhaa hiyo liko Afrika Mashariki ya Kati.
Akifafanua zaidi katika uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya chanjo na utambuzi wa mifugo kwenye uwanja wa Nyakabindi wilayani Bariadi mkoani Simiyu, waziri huyo amesema kuna fursa mpya kwa wafugaji na wawekezaji katika masoko ya Asia na China ambapo nyama inayohitajika ni tani 54,000.
Waziri Ashatu amesema Tanzania inatarajia kuingia katika soko la Ulaya kuuza nyama yake baada ya serikali kumaliza zoezi la upatikanaji wa cheti cha ithibati kutoka katika Shirika la Wanyama Duniani na kutatua changamoto zote za magonjwa nyemelezi kwa wanyama.
Ameongeza kuwa zoezi la chanjo kwa mifugo litarahisisha upatikanaji wa kibari cha kuuza nyama katika soko la Ulaya na masoko mengine.
Rais Samia Suluhu anatarajia kushiriki zoezi la kampeni ya chanjo na utambuzi wa mifugo pamoja na kuhitimisha kongamano la wafugaji 2025 mchana wa June 16 katika viwanja vya Nyakabindi pamoja na kuongea na wafugaji wote juu ya umuhimu wa chanjo kwa mifugo.
Januari 6, 2023, Msajili wa Bodi ya Nyama Tanzania (TMB), Dk Daniel Mushi alisema katika kipindi cha Novemba mwaka 2022, Tanzania iliuza nje ya nchi tani za nyama 1,423 zenye thamani ya Dola 5,370,187.70 sawa na zaidi ya Sh bilioni 10 za Kitanzania.