Mauzo ya asali nje yafikia tani 1,713 mwaka 2025

SERIKALI imesema mauzo ya asali nje ya nchi yameongezeka kutoka tani 607 za thamani ya Sh bilioni 4.8 mwaka 2021 hadi tani 1,713 za thamani ya Sh bilioni 18.6 mwaka 2025. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji amesema hayo wakati akifungua kikao cha wadau wa sekta za nyuki, misitu na malikale mkoani Dodoma.
Amesema ongezeko hilo limechochewa na jitihada mahususi za Rais Samia Suluhu Hassan za kuendelea kuhamasisha uwekezaji kwenye miradi ya upandaji miti na ufugaji nyuki. Kadhalika, amesema wizara kupitia taasisi zake za utafiti imeendelea kufanya tafiti mbalimbali zenye malengo ya kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya misitu na nyuki.
Amesema serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imechukua hatua madhubuti za kuandaa na kutekeleza mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kampeni ya kupanda miti milioni 1.5 kwa kila halmashauri kila mwaka. “Pamoja na hilo, kuendeleza pia mpango wa Tanzania ya kijani na kurejesha hekta milioni 5.2 za ardhi zilizoharibika kupitia mpango wa kurejesha maeneo Afrika,” aliongeza Dk Kijaji.
Aidha, Dk Kijaji amesema thamani ya mauzo ya mazao ya misitu nje ya nchi imeongezeka kutoka Sh bilioni 105 mwaka 2020/2021 hadi Sh bilioni 558.5 mwaka 2024/2025. Amesema ongezeko hilo linaenda sambamba na ongezeko la viwanda vya mazao ya misitu kutoka viwanda 636 mwaka 2021 hadi viwanda 1,671 mwaka 2025.
“Kama tunavyofahamu sekta zetu za misitu na ufugaji nyuki zinachangia takribani asilimia 3.5 ya pato ghafi la taifa letu. Kutokana na umuhimu wake, wizara imefanikiwa kuandaa mipango 235 ya kusimamia hifadhi ya misitu yetu,” aliongeza Dk Kijaji. SOMA: Nyuki wageuzwa kisima cha mapato, uhifadhi mazingira

Dk Kijaji ameeleza kuwa sekta za nyuki, misitu na malikale ni chanzo kizuri cha ajira rasmi na hata zisizo rasmi na kwamba zinachangia maendeleo ya jamii na uhifadhi endelevu wa mazingira. Ameongeza kuwa ili kupata asali iliyo bora kupitia Tanzania iliyo bora kwa kuhakikisha uzalishaji wa asali yenye viwango bora vya kimataifa unaohitajika sokoni unaimarishwa.
Amefafanua kuwa kupitia maboresho ya Sheria ya Mambo Kale Sura ya 333 kuruhusu ushiriki wa sekta binafsi katika uanzishwaji wa makumbusho binafsi, hadi sasa makumbusho tisa binafsi zimeanzishwa. Amesema katika mwaka 2024/2025 pekee, jumla ya maeneo 15 yametambuliwa na kukidhi vigezo vya kuwa urithi wa taifa na kwamba taratibu za kuyatangaza zinaendelea.
Kadhalika, alitanabaisha kuwa wadau wengine sita wameleta maombi ya muongozo wa na utaalamu wa kuanzisha makumbusho binafsi na matamasha ya kumbukumbu katika maeneo mbalimbali ya Tanzania. Amesema sekta hizo ni nguzo muhimu za uchumi wa nchi na kwamba zinachangia maendeleo jamii na uhifadhi endelevu wa mazingira.



