Mavunde aagiza dosari za uchimbaji zifanyiwe kazi Mwakitolyo
WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde amemuelekeza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo kufanyia kazi marekebisho ya dosari zote za kiusalama zilizopo katika eneo la Mwakitolyo mkoani Shinyanga.
Eneo hilo la Mwakitolyo lipo chini ya ubia wa msaada wa kiufundi (technical support), ambapo Mavunde ameagiza dosari zote za kiusalama zilizopo zirekebishwe, ili kuwaruhusu wachimbaji wadogo wafanye shughuli za uchimbaji katika mazingira ambayo ni rafiki.
Akizungumzia mkoani Shinyanga, Mavunde pia ametaka wachimbaji wadogo wasibugudhiwe na kupiga marufuku mchimbaji mdogo yoyote kuondolewa katika eneo lake kwa kuwa eneo hilo liligawiwa kwa wachimbaji wadogo kama wanufaika wa kwanza.
Mavunde ametoa maagizo hayo wakati akipokea taarifa ya ukaguzi uliofanywa na timu ya wataalamu aliyoiunda kuhusu uchambuzi wa mikataba kati ya vikundi vya wachimbaji wadogo wa madini na wabia (technical support) kwenye leseni za uchimbaji mdogo zilizopo katika eneo la Mwakitolyo mkoani Shinyanga.
Katika uchunguzi huo kamati imebaini sehemu kubwa ya maduara hayapo katika hali salama ya uchimbaji.
Akiwasilisha taarifa hiyo, Mwenyekiti wa timu ya watalaamu Mhandisi Ally Samaje amebainisha kwamba eneo la uchimbaji la Mwakitolyo linahitajika kukatwa kwa miamba inayoyoning’inia na kurekekebisha maduara, ili wachimbaji wachimbe kwa usalama zaidi na kuongeza uzalishaji kuliko ilivyo hivi sasa.