Mavunde aongoza kikao cha kimkakati wa kiuchumi kupitia STAMICO

SHIRIKA la Madini la Taifa (STAMICO) limekaa mguu sawa kuhamia kwenye uwekezaji mkubwa wa Madini Muhimu na Madini Mkakati.
STAMICO tayari imekuwa na mafanikio kadhaa ikiwemo kuachana na utegemezi kwa Serikali kwa asilimia 100 na likiwa limekwisha toa gawio kwa Serikali ya kiasi cha shilingi bilioni 9.
Mbali na hayo, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha shirika hilo linakua kubwa kama ilivyo malengo ya kuanzishwa kwake ya kuwekeza kwa niaba ya Serikali ambapo miongoni mwa majukumu yake ni kuwekeza kwenye miradi ya kimkakati ya utafutaji na uchimbaji madini ili kuongeza manufaa zaidi kwa taifa.
Hayo yamebainishwa zikiwa zimepita siku kadhaa tangu Bunge lipitishe Bajeti ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2025/26 ambapo miongoni mwa yaliyopangwa kutekelezwa mwaka ujao ni pamoja na kuzijengea uwezo taasisi zilizo chini ya Wizara pamoja na kuendeleza mnyororo wa thamani katika madini muhimu na mkakati.
Kikao hicho ni cha pili baada ya kikao cha kwanza kilichofanyika Mei 12, 2025 jijini Dodoma ambavyo vyote vimeongozwa na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde vikihusisha Menejimenti ya Wizara na Taasisi zake ili kujadili kwa pamoja andiko la kuiwezesha STAMICO) kuwekeza katika uchimbaji mkubwa wa madini nchini.
Awali, STAMICO liliwekwa kwenye orodha ya mashirika yanayopaswa kufutwa na Serikali na miaka ya karibuni, kupitia Falsafa ya 4 Rs za Rais Samia Suluhu Hassan Shirika limeweza kuishi mageuzi hayo kwa vitendo na kuweza kujipambanua kuwa miongozi mwa mashirika ya mfano yanayofanya vizuri na sasa limejikita kuwekeza katika shughuli za uchimbaji mkubwa na wa Kati wa madini muhimu na mkakati Pamoja.