NAIBU Waziri wa Kilimo ambaye pia ni Mbunge Jimbo la Dodoma Mjini Anthony Mavunde amekabidhi mashamba ekari nne mahsusi kwa kilimo cha mboga mboga na matunda.
Mashamba hayo yamekabidhiwa kwa vikundi vya wafanyabiashara wadogo wa Twiga Group-Soko la Sabasaba na Mavunde Garden-Soko Kuu Majengo jijini Dodoma.
Mavunde amekabidhi mashamba hayo katika mbuga ya Sogeambele,Kata ya Chihanga ikiwa ni utekelezaji wa mipango ya uwezeshwaji wananchi kiuchumi.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi mashamba hayo amesema ana imani kupitia mashamba hayo wafanyabiashara hao wadogo wataweza kuzalisha kwa wingi mazao ya mboga mboga na matunda na kuwa wasambazaji wakubwa wa mazao hayo ndani na nje ya mipaka ya Dodoma.
“Mashamba haya yakitumika vizuri yanaweza kuwa chanzo kikubwa cha mapato kwa vikundi vyenu na mimi nitakuwa nanyi bega kwa bega kuwapa msaada wowote unaohitajika ili muweze kufikia malengo yenu.”Amesema na kuongeza
“Pia nitawasaidia mbegu bora kwa mazao ambayo mtachagua kuyapanda,gharama za maandalizi ya shamba na pia nimezungumza na watu wa TAHA ili baadaye tupate vioski mwendo kwa ajili ya kuuzia mazao yetu.”Amesema Mavunde
Wakitoa shukrani zao viongozi wa vikundi hivyo Anna Nyigana (Twiga Soko Sabasaba) na Yona Msanganzila (Mavunde Garden Majengo Sokoni) wamemshukuru Mavunde kwa namna ambavyo amekuwa akiwawezesha kiuchumi na kuahidi kwamba watatumia mashamba hayo kuleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi katika vikundi vyao.