Mavunde awaita wawekezaji nchini

TANGA: WAZIRI wa Madini Anthony Mavunde amewakaribisha wawekezaji wa viwanda vya uzalishaji wa betri za magari ya umeme na vifaa vya kieletroniki kuwekeza nchini.

Mavunde amesema Tanzania imebarikiwa madini mkakati ya kutosha ambayo ni malighafi kuu ya uzalishaji wa betri za magari ya umeme na vifaa vya kieletroniki.

Ameyasema hayo Kwamsisi,wilayani Handeni mkoani Tanga wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanda cha uchenjuaji madini mkakati ya kinywe (Graphite) kinachomilikiwa na Kampuni ya Godmwanga Germs Ltd.

“Uwekezaji huu unatokana na mazingira mazuri na wezeshi yaliyowekwa na serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ” amesema Mavunde.

Aidha, amempongeza Mwekezaji Mtanzania God Mwanga kwa kuwa mmoja kati ya wawekezaji wakubwa wa madini kinywe nchini Tanzania na hivyo kuchochea ukuaji wa sekta ya madini na upatikanaji wa nafasi za ajira kwa watanzania.

“Mkakati wa serikali ni kuhakikisha madini haya yanaongezwa thamani nchini Tanzania ili kutunza ajira za watanzania,kuwajengea uwezo na kukuza uchumi wa taifa kupitia kodi na mapato mbalimbali.

“Hivyo niwakaribishe wawekezaji wote wenye nia ya kuongeza thamani mkakati haya kuitumia fursa hii kwa kuwa Tanzania imebarikiwa madini mengi na ya kila aina.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Handeni Wakili Albert Msando amesema mkakati mkubwa wa wilaya kwasasa ni kuhakikisha kunaku na umeme wa kutosha ili kuongeza uzalishaji katika mgodi huo.

“Kwasasa kuna mradi wa thamani ya Sh bilioni 60 wa ujenzi wa kituo kidogo cha kupooza umeme ambao utaelekezwa katika maeneo ya uzalishaji ikiwemo viwanda vya uchenjuaji wa madini sambamba na ukarabati wa miundombinu ya barabara, ” amesema Msando

Akitoa maelezo ya awali Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Godmwanga, God Mwanga amesema ujenzi wa kiwanda hicho ukikamilika utakuwa na uwezo wa uzalishaji wa tani 800 za madini kinywe kwa usiku na utakuwa unaingizia serikali zaidi ya Sh bilioni 1.8 kwa mwezi kama mapato yatokanayo na ada,tozo na mrahaba.

Habari Zifananazo

Back to top button