Mawakala wakwamisha usambazaji mbolea Iringa

HALMASHAURI ya Manispaa ya Iringa, imelazimika kutumia trekta lake la kusomba takataka kusambaza mbolea ya kupandia kwa wakulima wake wanaotakiwa kunufaika na pembejeo za ruzuku katika msimu huu wa kilimo.

Taarifa iliyotolewa hii leo na Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini Jesca Msambatavangu katika kikao cha Ushauri cha Mkoa (RCC), inaonesha uamuzi huo umefanywa baada ya baadhi ya mawakala kuingia mitini kwa sababu mbalimbali ikiwemo faida ndogo wanayopata katika biashara hiyo na hivyo kuathiri usambazaji wa mbolea kwa wakulima.

“Kuna changamoto nyingi ikiwemo pia ya matumizi ya teknolojia. Akina bibi wanakuja mjini kufuata mbolea na hawaipati kwa wakati kwa sababu ya matumizi ya teknolojia, tuiombe wizara iwe tayari kupokea ushauri ili changamoto hizo zimalizwe,” alisema na kusisitiza kwamba tatizo la kufikisha mbolea kwa wakulima ni kubwa sana.

Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego katika kikao hicho inaonesha mpaka sasa ni kati ya asilimia 30 na 33 tu ya mbolea ya kupandia ndiyo iliyofika kwa wakulima, wakati kuna shehena kubwa katika maghala ya kuhifadhia bidhaa hizo.

“Nilianza kupokea malalamiko kutoka kwa wabunge wakilalamika wakulima wao kukosa mbolea. Lakini taarifa zinaonesha mbolea zipo lakini shida ipo kwenye usambazaji, tulipouliza baadhi ya mawakala walilalamika malipo yao kuchelewa,” alisema.

Alisema baada ya kupokea taarifa hiyo waliifikisha serikalini na tayari taratibu za kuwalipa mawakala hao zinaendelea.

Aidha Mkuu wa Mkoa aliwashukia maafisa ugani akisema wengi wao wanashindwa kutimiza wajibu wao kwa sababu wamejigeuza kuwa watendaji wa kufuatwa ofisini badala ya wao kuwafuata wakulima.

Mbali na mbolea, alisema ni wajibu kwa kila kiongozi katika eneo lake kuhakikisha wakulima wake wanafikiwa na huduma, ili kuiongezea tija sekta hiyo ya kilimo ili ilete nafuu zaidi ya maisha kwa wananchi na kuchochea uchumi wao.

Wakati huo Mkuu wa Mkoa amesema pato la mtu kwa mwaka mkoani Iringa limeongezeka kutoka Sh Milioni 3.5 mwaka 2015 hadi Sh Milioni 4  mwaka 2020.

Aidha pato la mkoa kwa ujumla wake limeongezeka kutoka Sh Trilioni 3.5 mwaka 2015 hadi Sh Trilioni 4.6 mwaka 2020, ongezeko hilo likichangiwa na ukuaji wa kilimo cha chai, mazao ya misitu, ufugaji na viwanda mbalimbali vikiwemo vya maziwa, vyakula na kuchakata mazao ya misitu.

Habari Zifananazo

Back to top button