SHILINGI bilioni 3.4 za ushuru wa mazao ya uvuvi, sawa na asilimia 70.344 ya lengo la kukusanya Sh bilioni 4.8 zimekusanywa mkoani Mwanza katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/22.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Ofisa Uvuvi wa Mkoa wa Mwanza, Titus Kilo alipokuwa akitoa taarifa ya makusanyo ya mapato ya uvuvi kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa.
Alisema fedha hizo zilizokusanywa kwa halmashauri nane za mkoa zimetokana na ushuru wa mauzo ya uvuvi, leseni za uvuvi na za vyombo vya uvuvi.
Alisema hadi kufikia Septemba mwaka huu, jumla ya Sh 814,204,627 zilikusanywa ikiwa ni sawa na asilimia 14.
5 ya lengo la makusanyo ya Sh bilioni 5.6.
Alisema makusanyo hayo yanatarajiwa kuongezeka kuanzia Januari mwakani kutokana na na leseni za uvuvi na vyombo ambavyo hufikia kikomo cha matumizi yake Desemba ya kila mwaka.
Kwa upande wa ukuzaji viumbe kwenye maji, Kilo alisema kumekuwepo na changamoto ya mavuno ya samaki kutoka maji ya asili kushuka kila mwaka kutokana na changamoto za uvuvi haramu, mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa mazingira na ongezeko la shughuli za uvuvi ikilinganishwa na rasilimali zilizopo.
Alisema ingawa bado kuna fursa ya kuongezeka kwa mavuno ya samaki kutoka katika vyanzo vya maji ya asili lakini kuna kila dalili ya mavuno hayo kuzidi kupungua iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa.
“Hatua mojawapo ya kukabiliana na hali hii ni ufugaji wa samaki,” alisema.
Alisema mkoa baada ya kuona changamoto hiyo, ulianzisha mkakati wa kukuza uzalishaji endelevu wa samaki kibiashara kwa njia ya vizimba.
“Lengo ni kuviwezesha vikundi vya vijana kwa kuvipatia mahitaji muhimu ya kufuga samaki,” alisema na kuongeza kuwa kwa kuanzia mkoa ulipanga kuwezesha vikundi 35 vya vijana vyenye wanachama 350 kutoka halmashauri saba za Mkoa wa Mwanza.
Alisema hadi kufikia Agosti mwaka huu, Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela iliwezesha jumla ya vikundi viwili vya vijana Sh 91,598,000 kwa ajili ya ufugaji wa samaki kwenye vizimba.
“Halmashauri zingine zilishindwa kutekeleza mkakati huo kutokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani kuwa madogo,” alisema.