Mazingira wanahabari kuendelea kuboreshwa

DAR ES SALAAM; SERIKALI imesema itaendelea kuboresha mazingira ya kisera na kisheria, ili kuimarisha zaidi sekta ya habari nchini.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Thobias Makoba akifungua kongamano la uhuru wa vyombo vya habari na kujieleza kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye.

Akizungumza kwenye kongamano hilo lililoandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) kwa kushirikiana na Chama cha Wanasheria wa Marekani (ABA), Makoba amesema chini ya uongozi wa Rais Dk Samia Suluhu Hassan kumeshuhudiwa mabadiliko makubwa katika tasnia kiasi cha kutoa uhuru mkubwa wa vyombo vya habari na kujieleza.

“Chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan tumeona mageuzi makubwa kwenye sekta ya habari nchini. Serikali tunaamini kwenye ushirikiano na sio mashindano. Kama Serikali tupo tayari kupokea maoni ya kuboresha kwa maslahi ya tasnia hii,” amesema Makoba.

Kwa upande wake Mratibu wa THRDC, Wakili Onesmo Olengurumwa, amesema lengo la kongamano hilo ni kujadili sheria zinazosimamia vyombo vya habari na Uhuru wa kujieleza na kubainisha changamoto.

Amesema THRDC wameshafanya uchambuzi wa kesi 30 na kubaini kuwa Sheria ya Makosa ya Mtandao, inaongoza kwa kuvunja haki ya kujieleza, kwani imepeleka watu wengi mahakamani kwa tuhuma za makosa ya uchochezi na kusababisha taharuki.

“Sheria ya Makosa ya Mtandao imevunja sana haki ya kujieleza, watu wanakamatwa hovyo bila kufuata utaratibu. Hivyo tumetoa mapendekezo yetu ya namba ya kuboresha Sheria zetu. Tunahitaji kuundwa kwa tume ya pamoja ili kuzifanyia marekebisho ziendane na wakati,” amesisitiza Wakili Olengurumwa.

“Tunapoelekea kwenye uchaguzi ni wakati wa kuwa na uhuru wa kweli na wazi, kwani bila hivyo wananchi watashindwa kutoa maoni yao,” ameeleza Wakili Olengurumwa.

 

Habari Zifananazo

Back to top button