PARIS, Ufaransa: TETESI kutoka vyombo mbalimbali vya habari barani Ulaya vinaeleza kuwa nyota wa klabu ya Paris St-Germain (PSG), Kylian Mbappe amekubali kujiunga na Real Madrid majira ya kiangazi.
Nahodha huyo wa Ufaransa (25), ameweka wazi dhamira yake ya kutaka kuondoka kwenye klabu hiyo baada ya mkataba wake kufikia ukingoni mwezi Juni.
Mbappe bado hajasaini mkataba na klabu ya Real Madrid, lakini anaweza kutangazwa kuwa mchezaji wa miamba hiyo ya soka ya Hispania kama hakutakuwa na uwezekano wa timu hiyo kukutana na PSG kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mshindi huyo wa Kombe la Dunia ameifungia PSG mabao 244 na kuwa mfumania nyavu bora wa wakati wote wa klabu hiyo yenye maskani yake katika Jiji la Paris.
Mbappe alitaka suala hilo likamilishwe kabla ya mwezi Machi, hivyo Februari 13 alikutana na Rais wa PSG, Nasser Al-Khelaifi na kumueleza kuwa anaondoka na anajiunga na klabu ya Real Madrid.
Baada ya taarifa kuibuka Alhamisi kwamba ataachana na klabu hiyo, Mbappe aliachwa kwenye kikosi cha kwanza kwa ajili ya mechi dhidi ya Nantes Jumamosi lakini aliingia akitokea benchi na kufunga bao la penalti lililoifanya PSG kuongoza Ligi Kuu Ufaransa kwa tofauti ya pointi 14.
Anatarajia kusaini mkataba wa miaka mitano na Real Madrid, utakaomfanya kulipwa euro milioni 15 sawa na pauni milioni 12 kwa msimu sambamba na ada ya uhamisho ya euro milioni 150 sawa na pauni milioni 128 ambayo italipwa kwa kipindi cha miaka mitano.
Kama kiungo wa kimataifa wa Croatia, Luka Modric ataondoka mwishoni mwa msimu huu, Mbappe atapewa jezi nambari 10 anayoivaa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa.