Rushwa yatajwa michezoni

DAR ES SALAAM: VITENDO vya rushwa vimetajwa kuwa miongoni mwa changamoto kubwa zinazoathiri maendeleo ya michezo nchini, hasa katika maeneo ya usajili wa wachezaji, upangaji wa matokeo ya mechi na uchezeshaji wa michezo.

Hayo yameelezwa na Ofisa na Mkuu wa Uelimishaji Umma wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kutoka Ilala, Mary Mwakyusa, wakati wa semina ya waandishi wa habari za michezo iliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA).

Amesema kumekuwa na matukio ambapo baadhi ya watu hupokea hongo ili kupindisha taratibu za michezo na kutoa upendeleo kwa timu fulani.

“Rushwa katika michezo ipo na inaathiri haki na ushindani wa kweli. Ni jukumu la kila mdau kushirikiana kuikomesha,” amesema Mwakyusa.

Ameongeza kuwa mapambano dhidi ya rushwa si jukumu la TAKUKURU pekee, bali yanahitaji ushiriki wa wadau wote wa michezo wakiwemo waandishi wa habari, ambao wanapaswa kuzingatia sheria na maadili ya taaluma yao.

Katika semina hiyo, Mwenyekiti wa TASWA Amir Mhando amesema kuwa bado kuna changamoto ya upungufu wa habari za kiuchunguzi katika michezo, hali inayochangia kutofichuliwa kwa baadhi ya vitendo visivyo halali.

Amesema kwa kutambua hilo wamewaleta wataalamu na magwiji wa habari ili kuwajengea uwezo waandishi katika uandishi wa habari za uchunguzi, wakiamini hatua hiyo itasaidia kuimarisha tasnia ya habari za michezo.

Aidha, matumizi ya teknolojia ya akili unde (AI) ametaja kuwa na changamoto na fursa, huku waandishi wakihimizwa kuitumia kwa uangalifu na weledi.

Mbali na TAKUKURU, wadau wengine waliowasilisha mada ni pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wakielezea majukumu yao na umuhimu wa uelewa wa masuala ya kodi kwa waandishi wa habari za michezo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button