Mbaroni akidaiwa kutusi viongozi
JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limemkamata mkazi wa Kigamboni, Selemani Agai Gaya (18) ambaye anatuhumiwa kutoa lugha za matusi kwa viongozi wa serikalini kupitia mtandao wa kijamii wa Tiktok
Akizungumza na waandishi leo jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi kanda hiyo, SACP. Jumanne Muliro amesema wamemkamata mtuhumiwa huyo akiwa na wenzake wakitengeneza maudhui ya video na kuzisambaza kwenye mitandao mengine ya kijamii zenye kuwatukana na kuwafedhehesha viongozi wa serikali.
Kamanda Muliro amesema mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani hivi karibuni, aidha ametoa onyo kali kwa watu wanaotoa lugha za matusi na fedheha kwa viongozi wa serikali kwa njia yoyote.
Amesema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za kisheria limejipanga kuwafuatilia, kuwakamata, kuwahoji na kuhakikisha wanafikishwa kwenye nyombo vya sheria.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Julai 31, 2023 limewakamata watuhumiwa saba akiwemo Amani Kipolo mkazi wa Vingunguti kwa tuhuma za kumshambulia na kusababishia kifo Hadija Hamisi na kuwajeruhi watu wengine nane.
Watuhumiwa hao wakiwa na wenzao kwenye kundi waliwashambulia wananchi mtaani maeneo ya Vingunguti kwa lengo la kulipiza kisasi wakati wakitoka kumzika mwenzao aliyefahamika kwa jina la Nurdin Bwino.
Bwino aliuawa kwa kushambuliwa na wananchi alipokuwa na wenzake sita wakiwa na visu na vifaa mbalimbali vya kuvunjia alipojaribu kuvunja nyumba moja usiku wa Julai 30, 2023.