Mbaroni kwa kutupa mtoto wa siku tatu

JESHI la Polisi mkoani Mwanza limemkamata Priska Lameck (28) akituhumiwa kumtupa mtoto wa umri wa siku tatu.

Mtoto huyo aliokotwa na msamaria mwema Februari 20 mwaka huu saa 12 asubuhi katika eneo la Buswelu Manispaa ya Ilemela.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mtafungwa alisema mama huyo ni mkazi wa Nyakato katika Wilaya ya Nyamagana.

Kamanda Mtafungwa alisema baada ya mahojiano mtuhumiwa huyo alikiri kufanya ukatili huo kwa madai kuwa alifanya hivyo kutokana na ugumu wa maisha.

Alisema Jeshi la Polisi limeendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali wakiwamo wanafunzi zaidi ya 3,000 kwa lengo la kudhibiti vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.

“Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani mara baada ya uchunguzi kukamilika,” alisema Kamanda Mtafungwa.

Alisema pia polisi walimkamata mtuhumiwa sugu wa makosa ya unyang’anyi na uvunjaji katika nyumba za watu, Lucas Mussa (24) ambaye pia ni mkazi wa Mtaa wa Mbege, Mkolani wilayani Nyamagana.

Kamanda Mtafungwa alisema mtuhumiwa huyo pia alikuwa akitafutwa na Jeshi la Polisi kwa kuhusika kwenye matukio mengi ya kiuhalifu.

Alisema Februari 21 mwaka huu, mtuhumiwa huyo alihusika kuvunja nyumba ya Josephina Leonard (28) ambaye ni mkazi wa Kahama katika manispaa ya Ilemela.

Aidha, Kamanda Mtafungwa alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa akiwa na vitu vya wizi vikiwemo runinga mbili, subwoofer mbili, betri mbili, CPU moja aina ya Dell na vifaa vya kuvunjia milango.

Habari Zifananazo

Back to top button