Mbaroni akidaiwa kuwadanganya Zimamoto

JESHI la Zimamoto na Uokoaji mkoani Geita, linamshikilia Shedida Ibrahim mkazi wa Mtaa wa Mkoani mjini Geita, kwa kosa la kupiga simu na kutoa taarifa za uongo kuwa kuna nyumba inaungua.

Akitoa taarifa hiyo leo, Ofisa wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Inspekta Edward Lukuba, amesema mtuhumiwa alitenda kosa hilo jana Septemba 5, 2022 saa moja usiku, baada ya kupiga simu ya dharura 114 na kujitambulisha kama Bi. Rehema.

“Alipiga simu kwa hisia kwamba kuna nyumba inaungua moto, askari wetu walitoka kuelekea kwenye tukio la moto, baada ya kukaribia tukio la moto yule dada alizima simu, hakupatikana tena,” amesema.

Advertisement

“Lakini leo Septemba 6, 2022 kupitia askari wetu makachero tuliweza kumbaini na sasa tuko naye kituo cha zimamoto Geita, ametupa ushirkiano,” amesema na kuongeza:

“Tumeangalia namba yake amekuwa ni miongoni mwa watu ambao wamekuwa wakipiga simu, lakini hawatoi ushirikiano wowote, kama wiki mbili nyuma tulipata namba yake kwenye orodha ya wapigaji simu.

“Leo pia tumelibaini hilo, tumefanya naye mahojiano na amekiri mwenyewe kwamba anafanya hivo kwa kujifurahisha na kujichangamsha,” ameeleza Inspekta Lukuba.

Amewataka wananchi wa Geita kutumia namba ya dharura  114, kwa kuomba huduma ya kuzima moto au uokoaji na siyo kwa kutoa wito wa uongo.

Amesema Kanuni za Mwaka 2008 za Ukaguzi wa Tahadahari na Kinga ya Majanga ya Moto, inaeleza watu wanaobainika kutoa taarifa za uongo adhabu yao ni kulipa faini ya Sh milioni tatu au jela miezi 12.

Kwa upande wake Shedida akizungumza na Daily News Digital, alikiri kupiga simu na kwamba hiyo ni mara yake ya kwanza.

“Nilijisikia tu kushika simu na kupiga simu, hii ni mara yangu ya kwanza kufanya hivi, sijawahi kupiga simu ya zimamoto,” alisema.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *