Vodacom yaipiga jeki ‘Twende Butiama’ kuboresha huduma za jamii

ARUSHA: Kampuni ya mawasiliano nchini, Vodacom Tanzania PLC, imetangaza udhamini wake kwa mbio za baiskeli ‘Twende Butiama 2o25’ kwa leno la kuchochea maendeleo endelevu katika jamii.

Mwaka huu, mbio hizo zitahusisha umbali wa takribani kilomita 1,500 ambao mikoa 11 itashuhudia mashindao hayo kuanzia Julai 3 na kutamatika Julai 13, mwaka huu.

Mbio hizo zitamalizika kwa kishindo katika kijiji cha Butiama mkoani Mara – mahali alipozaliwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere

Advertisement

Akizungumzia kuhusu msafara huo, Mkurugenzi wa Uhusiano na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania na Vodacom Tanzania Foundation, Zuweina Farah, alisisitiza dhamira ya kampuni hiyo kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma katika harakati za maendeleo nchini.

“Tunaamini katika kuunganisha Watanzania kwa mustakabali bora, na Twende Butiama ni moja ya njia tunayoitumia kutimiza dira hiyo. Iwe ni ujumuishaji wa kidijitali, upatikanaji wa elimu, huduma bure za afya au utunzaji wa mazingira, kampeni hii inaonesha nguvu ya ushirikiano na dhamira ya kweli,” alisema Zuweina.

Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Twende Butiama imeboresha maisha ya maelfu ya Watanzania. Zaidi ya watu 150,000 wamenufaika na huduma za afya bure, zaidi ya miti 100,000 imepandwa katika shule mbalimbali nchini na kuhamasisha uelewa wa mazingira na kuboresha mazingira ya kujifunzia, zaidi ya madawati 1,900 yamegawiwa kwa shule za msingi 34 ili kupunguza idadi ya wanafunzi kukaa chini, na baiskeli 50 zimesambazwa kwa wanafunzi wa vijijini ili kuwapunguzia muda wa kufika shuleni na kuongeza mahudhurio.

Waendesha baiskeli 200 kumuenzi Nyerere

Msafara wa mwaka huu unaendeleza mafanikio hayo kwa kuzingatia zaidi upatikanaji wa elimu jumuishi, uhifadhi wa mazingira, na utoaji wa huduma bora za afya.

Aidha, kampeni hiyo itaendelea kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum kwa kugawa vifaa vya kusaidia kama vile viti, kwa lengo la kujenga jamii jumuishi. Msafara huo utaanza rasmi katika viwanja vya Kijitonyama jijini Dar es Salaam na kwa mara ya kwanza zitapitia mikoa ya Pwani, Tanga, Arusha, Manyara, Singida, Tabora, Shinyanga, Simiyu hadi Mara.

Katika maeneo haya, waendesha baiskeli, wadau na wanajamii watahusika moja kwa moja katika shughuli za upandaji miti, msaada wa kielimu, kambi za afya na usafi wa mazingira. Mwanzilishi wa msafara wa Twende Butiama, Gabriel Landa, alisema: “Kilichoanza kama harakati ndogo za baiskeli sasa kimekuwa harakati ya kitaifa ya kuleta mabadiliko.

“Kila mwaka tunapanda miti, tunatoa elimu, na kugusa maisha ya maelfu ya Watanzania. Safari ya mwaka huu kutoka Dar es Salaam hadi Butiama ni safari ya matumaini kwa taifa letu.”

Msafara wa Twende Butiama unadhaminiwa na wadau kadhaa wakiwemo ABC Impact, ABC Bicycle, serikali za mitaa, vilabu vya baiskeli vya kitaifa na kikanda pamoja na mashirika ya maendeleo.

Vyombo vya habari vinatarajiwa kuwa sehemu muhimu katika kufikisha simulizi, sauti, na nyuso za wanufaika wa msafara wa Twende Butiama.

2 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *