Mbio kutangaza historia ya Mwalimu Nyerere

TAASIS ya Makumbusho ya Taifa imeandaa mbio za hiari maarufu kama “Nyerere Marathon” kwa lengo la kutangaza historia ya Mwalimu Julius Nyerere zinazotarajiwa kufanyika Butiama mkoani Mara.

Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho, Dk Noel Lwoga amesema hayo jana Dares Salaam na kuongeza kuwa mbio hizo zinatarajiwa kufanyika Septemba 30,2023.

Amesema mbio hizo zina lengo la kutangaza historia ya Nyerere kukuza utalii wa ndani na kuhamasisha mazoezi ya viungo ili kujenga afya njema na kuongeza kipato kwa jamii na mtu mmoja mmoja.

Amesema kwa mwaka huu wa 2023 mbio hizo pia zinalenga kukusanya fedha na vifaa kwa ajili ya kuandaa na kuweka onesho maalumu kwaajili ya watu wenye mahitaj maalum wakiwemo wasioona na wenye uono hafifu kwa kutumia matumizi ya sauti na nukta nundu katika Makumbusho ya Mwl. Nyerere Butima.

Amesema mbio hizo ni za kipekee kwa sababu zinahusisha siku, mwezi na mwaka aliozaliwa Mwalimu Nyerere yaani Aprili 13, 1922.

“Hivyo kutakuwa na mbio za kilomita nne, 13 na 22 na njia kuu itakayotumika katika mbio hizo ni barabara ya Butiama kwenda Busega ambayo Hayati  Mwalimu Nyerere alitumia kwenda shule ya msingi kila siku na kurudi nyumbani,” amesema.

Aidha amesema barabara ya Butiama – Busega ina miinuko mingi ambayo hupendelewa sana na wanariadha.

Dk Lwoga amesema gharama za ushiriki wa mbio hizo ni Sh.30,000 tu kwa watu wazima na wanafunzi ni sh 5,000 kwa mwaka huu wa 2023 inataraja kuwa na washiriki zaidi ya 5,000.

Amesema zawadi kwa washindi kwa kila umbali zitatolewa kuanzia mshindi kwanza hadi wa 10 zawadi ni tofautitofauti kuanzia sh milioni moja Hadi sh 50,000. Amesema kwa watoto wenye mahitaji maalumu watakaoshiriki watapata zawadi maalum kila mmoja.

Habari Zifananazo

4 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button