Mbio za kusaka mil 10/- za Vunjabei Cup zakolea Iringa

Vunjabei Cup 2025 imevunja historia mkoani Iringa kwa kuweka zawadi kubwa ya Sh milioni 10 kwa mshindi wa kwanza, ikiwasha moto mpya wa ushindani na kuongeza thamani ya mashindano ya chini ya mpira wa miguu.

Kwa miaka mingi, Iringa imekuwa ikishuhudia mashindano ya soka katika ngazi za kata, huku mengi zawadi zake za juu kabisa ikiwa mbuzi wa Sh 150,000 seti ya jezi, na mpira.

Yakiungwa mkono, mashindano haya yanaweza kuwa chachu ya kuinua hali ya michezo mkoani Iringa, kuibua vipaji vipya, na wananchi wake kurudisha mapenzi ya soka linalozidi kuporomoka ikiwemo timu ya Lipuli FC iliyowahi kushiriki ligi kuu nchini kushuka hadi daraja la tatu.

Advertisement

Michuano hii ya Vunjabei Cup imeingia hatua ya pili na ya mwisho inayozikutanisha timu bora 50 zilizofuzu kutoka ngazi ya awali iliyoanza rasmi Januari 11, 2025.

“Katika hatua hii timu zote 50 tunazipa vifaa maalum vya michezo vitakavyotumika kwenye safari yao ya kusaka ubingwa wa Vunjabei Cup 2025,” alisema Mkurugenzi wa Vunjabei Fredy Ngajilo.

“Tunatambua kuwa michezo si burudani tu, bali ni afya na ajira. Tunaleta mashindano haya ili kuwapa vijana wetu fursa ya kuonyesha vipaji vyao na kujitengenezea mustakabali mzuri wa maisha,” alisema Ngajilo kwa bashasha.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, bingwa wa Vunjabei Cup 2025 ataondoka na kitita cha Shilingi milioni 10, kiasi kinachozidi kuongeza hamasa kwa wachezaji na mashabiki.

Uzinduzi wa hatua hii ya timu 50 bora ulizikutanisha katika uwanja wa Kalenga, Kalenga FC na Mgela FC, ambao ulimalizika kwa sare ya 1-1.

Hadi filimbi ya mwisho, timu zote zilionyesha mchezo wa hali ya juu, zikithibitisha kuwa ushindani kwenye Vunjabei Cup 2025 umefikia viwango vya juu.

Mbali na mpambano mkali wa uwanjani, uzinduzi wa hatua ya makundi uligeuka kuwa tamasha la burudani baada ya Stamina, Dulla Makabila, na Eze Nice kuwapagawisha mashabiki kwa nyimbo zao kali.

Stamina, akitamba na mashairi yake makali, alihamasisha vijana kuhusu umuhimu wa kujituma na kutumia vipaji vyao ipasavyo.

Dulla Makabila, kwa mtindo wake wa Singeli, aliwafanya mashabiki kusahau uchovu wa mechi na kuingia kwenye mzuka wa densi, huku Eze Nice akihakikisha mashabiki wa Iringa wanajivunia burudani kutoka kwa msanii wao wa nyumbani.

Mratibu wa mashindano hayo yanayosimamiwa na Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Iringa, Fadhili Ngajilo, amesema kuwa iwapo mashindano haya yatapata mafanikio makubwa, kuna mpango wa kuyapanua hadi mikoa jirani.

“Tumeshuhudia mwitikio mkubwa kutoka kwa vijana na mashabiki wa soka. Kama Vunjabei Cup 2025 itaendelea kwa mafanikio haya, tunapanga kuyaeneza hadi mikoa mingine ili kutoa nafasi kwa vipaji vipya zaidi kung’aa,” alisema Fadhili Ngajilo.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *