Mbio za Mtembezi kuvutia washiriki 500 Iringa

KATIKA juhudi za kuhamasisha utalii wa ndani na kuchochea ukuaji wa uchumi, mbio za kipekee zinazojulikana kama “Mtembezi Marathon” imeandaliwa kwa mara ya kwanza mjini Iringa, kitovu cha utalii kusini mwa Tanzania.

Akizungumza na wanahabari Mkurugenzi wa Mtembezi Adventures inayoandaa na kuratibu mbio hizo, Samson Samwel Mtembezi Marathon itakayofanyika Desemba 7 mjini Iringa inatarajia kuvutia zaidi ya washiriki 500.

Amesema wameleta mbio hizo Iringa kwa kuwa ni moja ya mikoa ambayo imejipatia sifa kwa kuwa na vivutio mbalimbali vya utalii vikiwemo vya utamaduni na historia, mandhari na kilimo, na vivutio vya asili ikiwemo hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Advertisement

“Mbio hizi zinaweza kuhusisha maeneo ya kihistoria ndani ya mji wa Iringa, kama Kanisa la Kale la Wamisionari wa Kilutheri na soko la mji ambalo lina bidhaa za sanaa na ukumbusho wa kitamaduni,” alisema.

Alisema wanataka kuona mbio hizo, ambazo tayari zimekusanya washiriki kutoka maeneo mbalimbali nchini, zinakuwa kivutio kikubwa kwa watalii wa ndani na nje ya nchi, huku zikionesha uzuri wa asili na urithi wa kitamaduni wa Tanzania.

Alisema lengo kuu la mbio hizo ni kuwahamasisha watanzania kuchangamkia utalii wa ndani na kuelewa umuhimu wake katika kukuza pato la Taifa.

“Mbio hizi zinalenga kuhamasisha wananchi kutembelea mbuga za wanyama, milima, na vivutio vingine vya kipekee ambavyo mara nyingi hutembelewa na wageni wa kimataifa pekee,” alisema na kuongeza marathon hiyo itakuwa ya kilomita 5, 10, na 21.

Marathon hiyo alisema itafungua fursa kwa wajasiriamali wa ndani, huku mahoteli, migahawa, na biashara ndogondogo zikishuhudia ongezeko la wateja na sehemu ya mapato yatakayokusanywa kutokana na ada za usajili na udhamini yatarudishwa kwa jamii.