Mbivu mbichi kujulikana leo Kenya

KENYA : WABUNGE nchini Kenya wanatazamiwa kuwasilisha hoja ya kumg’oa madarakani Naibu Rais Rigathi Gachagua katika bunge la taifa leo Oktoba 1.

Kiongozi wa wengi na mbunge wa Kikuyu, Kimani Ichung’wah alithibitisha kuwa hoja dhidi ya Gachagua itawasilishwa mbele ya Bunge saa nane mchana kwa saa za Afrika mashariki.

Uwasilishaji wa hoja hiyo utahitaji kuungwa mkono na wabunge 233 na kuna taarifa zinazodai kuwa wajumbe 302 tayari wametia saini.

Wanaomshitaki Gachagua wanadai kuwa amekiuka Kifungu cha 10 cha katiba, wakisema matamshi yake hadharani yamekuwa ya uchochezi na yanaweza kuibua chuki za kikabila.

Pia anatuhumiwa kukiuka vifungu vya sheria vinavyozungumzia mwenendo na wajibu wake kama msaidizi mkuu wa Rais.

Gachagua atajitetea dhidi ya madai ya kujipatia mali kwa ufisadi na kutumia pesa za walipa kodi kwa njia isiyo halali ambapo  mali hiyo inasemekana kusambazwa katika kaunti za Nyeri, Nairobi na Kilifi.

Ikiwa hoja hiyo itakamilika, Spika wa bunge la taifa, Moses Wetangula atawasilisha azimio hilo kwa spika wa bunge la seneti Amason Kingi ndani ya siku mbili ili achukuliwe hatua.

SOMA:Polisi yatawanya wabunge walioandamana ofisi ya Ruto

Hoja ya kumuondoa madarakani Gachagua inakuja huku kukiwa na uhusiano mvutano baina yake Rais William Ruto ambapo viongozi hao wawili wamekuwa wakitupiana lawama kila mmoja akidai mwenzake anakwamisha utendaji wa mwenzake.

Habari Zifananazo

Back to top button