Mbunge ahoji CAG aagizwe akague Saccos ya Polisi

DODOMA; MBUNGE wa Ndanda, Cecil Mwambe ameuliza swali bungeni kwa ni Serikali isiagize Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), akague URA SACCOSS ya Jeshi la Polisi.
Akijibu swali hilo bungeni leo Juni 4, 2025, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo, amesema URA SACCOSS ni chama cha ushirika kilichosajiliwa na kinasimamiwa na kukaguliwa kwa mujibu wa sheria ya vyama vya ushirika namba 6 ya mwaka 2013 na sheria namba 10 ya mwaka 2018 ya huduma ndogo ya fedha na ni mali ya wanachama ambao ni watumishi wa Jeshi la Polisi.
“URA SACCOSS hukaguliwa kila mwaka na shirika la ukaguzi na usimamizi wa vyama vya ushirika COASCO, pia hukaguliwa na mrajisi wa vyama vya ushirika kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika TCDC.
“URA SACCOSS ni ushirika uliopata hati safi kuanzia mwaka 2015 hadi 2024, pia umepata tuzo ya saccoss bora nchini kuanzia mwaka 2021 hadi 2024, hii ni kutokana na kufuata sheria, kanuni na taratibu za ushirika na fedha na taarifa zake husomwa kwenye mkutano mkuu wa mwaka wa wanachama kama matakwa ya sheria yanavyoelekeza,” amesema Naibu Waziri.