Mbwa washambulia mtoto Katavi

WATU wawili akiwemo mtoto mwenye umri wa miaka sita wakazi wa Mtaa wa Maridadi, Kata ya Majengo, Manispaa ya Mpanda mkoani Katav,i  wamenusurika kifo baada ya kushambuliwa na mbwa anayedaiwa kuwa na kichaa katika maeneo mbalimbali ya miili yao.

Matukio hayo ambayo yanadaiwa kutokea kwa nyakati tofauti, yameibua hofu kwa wananchi wa Manispaa ya Mpanda kutokana na mbwa wengi kuzagaa mtaani.

Wakizungumza katika mkutano wa Diwani wa Kata ya Majengo, waathirika Said Mustapha na Grace Baltazali ambae ni dada wa mtoto huyo, wameomba msaada kwa serikali ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua za haraka kwa mbwa wanaozagaa mtaani.

Naye Diwani wa Kata ya Majengo, William Mbongo amewataka wananchi kutoa taarifa sehemu husika pale wanapoona mbwa mwenye dalili ya kichaa, huku Mwenyekiti wa Mtaa wa Maridadi Donatha Mpandangazi, akisema kuwa mtaa wake watu wawili wamepatwa na tatizo hilo.

Kwa upande wake Katibu wa Hospitali ya Manispaa ya Mpanda, Siame Wambote, amesema mpaka sasa wamepokea mgonjwa mmoja aliyeumwa na mbwa na anaendelea na matibabu katika hospitali hiyo.

“Tumempokea mtoto Beritha Baltazali mwenye umri wa miaka 6, alikuja akiwa amejeruhiwa maeneo ya kichwani,mkononi na mguuni, ambapo tumempatia matibabu na sasa anaendelea vizuri,” amesema.

 

Habari Zifananazo

Back to top button